Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

11 Februari 2021

12:53:30
1114306

Maadhimisho ya Bahman 22, nembo ya umoja na nguvu laini za taifa la Iran mbele ya maadui

Leo Jumatano, Februari 10, 2021 zimefikia kileleni sherehe za Bahman 22 za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Sherehe hizo ni kumbukumbu ya moja ya matukio muhimu sana katika historia ya taifa la Iran. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi tarehe 11 Februari 1979 kwa uongozi wa mwanachuoni shujaa, Imam Khomeini MA.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wananchi wa kona zote za Iran bali hata wapenzi wa Jamhuri ya Kiislamu nje ya Iran huadhimisha kwa shauku kubwa sherehe za Bahman 22 kila mwaka. Kila mwaka wananchi katika kona zote za Iran wanashiriki katika maandamano ya mamilioni kwa hamasa na shauku kubwa katika kilele cha sherehe hizo ili kutangaza utiifu wao kwa Jamhuri ya Kiislamu na kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ijapokuwa mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kwa sura nyingine kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona, lakini hamasa na shauku kubwa ya wananchi imeendelea kuonesha uhai na kuendelea kuwepo matukufu ya Mapinduzi hayo.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umekuwa sababu ya mabadiliko makubwa na muhimu sana kwa taifa la Iran na katika kudhihiri fikra mpya za kimampinduzi zilizosimama juu ya msingi wa matukufu ya Mwenyezi Mungu katika mapambano ya mataifa mbalimbali duniani dhidi ya dhulma na ukandamizaji. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu uliliokoa taifa la Iran kutoka kwenye makucha ya kujidhalilisha na kutegemea madola ya kiistikbari na kuliingiza taifa hili katika njia ya kufikia kwenye uhuru, heshima na maendeleo katika nyuga zote.

Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran yametoa taathira kubwa sana pia kwa mataifa yanayodhulumiwa na yanayokandamizwa duniani na yamekuwa sababu ya mabadiliko makubwa katika mwamko wa Kiislamu na kuundika kambi ya muqawama ya kupambana na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume Muhammad SAW na siku ya kuzaliwa Imam Jafar al Sadiq AS alisema, sababu kuu ya uadui wa Marekani kwa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo huo wa Kiislamu kutokubali kuburuzwa na siasa za kidhalimu na kutoutambua kwake ubeberu wao. Alisisitiza kuwa: Uadui huu utaendelea kuwepo na njia pekee ya kupambana nao ni kumlazimisha adui akate tamaa na afute njozi yake kwamba anaweza kutoa pigo la kimsingi kwa taifa na serikali ya Iran.

Aidha amesema: Mabeberu kama wanavyosema wenyewe, wanataka kuifanya Iran iwe nchi ya kawaida, yaani iendane na vile wanavyotaka mabeberu, lakini Jamhuri ya Kiislamu tangu ilipoasisiwa hadi leo hii, imesimama imara kukabiliana na mfumo wa kibeberu na katika siku za usoni pia kamwe haitosalimu amri mbele ya uistikbari wa kimataifa, bali itaendelea njia ya kimapinduzi ya kukabiliana na mabeberu bila ya kutetereka. 

Kigezo hicho ni sehemu ya madhihirisho ya heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo ni matunda ya juhudi na kujitoa muhanga mashahidi kama vile Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Kutokana na ushindi mbalimbali mkubwa ulioongozwa na shujaa huyo katika medani za kupambana na maadui, Luteni Jenerali Qassem Soleimani alifanikiwa kufelisha njama za Marekani na Israel za kutaka kuzigawa vipande vipande nchi za ukanda huu. Vile vile alifanikiwa kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo hili. Mabadiliko hayo makubwa ni uthibitisho wa usafi, uimara na kuwa hai Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yamesimama imara kukabiliana na mabeberu wa dunia na kutetea wanyonge na mataifa yanayodhulumiwa duniani.

Maadui wa taifa la Iran walikuwa na ndoto kwamba kwa kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu na kufanya mauaji ya kigaidi dhidi ya wasomi na wanamapambano wa taifa hili wataweza kutoa pigo kwa Mapinduzi na kwa Jamhuri ya Kiislamu na kulifanya taifa la Iran liachane na malengo yake matakatifu, lakini Iran ya Kiislamu si tu haikutetereka, bali nguvu za Jamhuri ya Kiislamu zimeidi kuwa kubwa katika eneo la Asia Magharibi kiasi kwamba kusimama imara wananchi wa Iran mbele ya mashinikizo  ya kiwango cha juu ya maadui, kumekuwa ni nembo ya nguvu na heshima kwa Jamhuri ya kiislamu. Leo hii Iran ya Kiislamu inazidi kupiga hatua za kimaendeleo katika nyuga zote licha ya kuweko vitisho na mashinikizo ya kila namna.

342/