Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Machi 2021

08:05:09
1121321

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:

Kiongozi na Marjaa wa Waisalmu wa Madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani amekutana na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani katika mji mtakatifu wa Najaf, Iraq.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:Kwa mujibu wa taarifa katika mkutano huo wa Jumamosi, viongozi hao wamejadili kadhia ya Palestina na umuhimu wa wafuasi wa dini mbali mbali kuishi kwa maelewano.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Ayatullah Sistani imesema katika mkutano huo wa kihistoria, wawili hao wamezungumzia  changamoto zinazoikabili jamii ya mwanadamu wa leo na nafasi ya imani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na masuala ya maadili na changamoto zilizopo kuhusiana na maudhui hizo. 

Hakuna kiongozi wa kisiasa au afisa wa serikali ya Iraq aliyeshiriki katika mazungumzo hayo.

Katika kikao hicho, Ayatullah Sistani ameashiria matatizo na masaibu yaliyopo katika nchi za Asia Magharibi kama vile vita, vikwazo vya kiuchumi, watu kufurushwa makwao na hasa yanayojiri Palestina.

Taarifa hiyo imesema Ayatullah Sistani amesisitiza umuhimu wa viongozi wa kidini katika kutatua matatizo yaliyopo. Aidha imearifiwa kuwa Ayatullah Sistani alisisitiza kuhusu jitihada za kustawisha thamani kama vile watu kuishi pamoja kwa amani na pia wafuasi wa dini mbali mbali kuheshimiana.

Mwanazuoni na kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Kiislamu nchini Iraq aidha amesisitiza kuhusu raia Wakristo nchini Iraq kuishi kwa amani kama Wairaqi wengine na haki zao za kikatiba ziheshimiwe.

Nayo taarifa ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, imesema mkutano huo ulidumu kwa muda wa dakika 45 ambapo Papa Francis alimshukuru Ayatullah Sistani na Jamii ya Mashia kwa uungaji mkono wao kwa wanaodhulumiwa na pia kwa kutetea umoja wa Iraq.

Papa Francis pia amesisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano,urafiki na mazungumzo baina ya wafuasi wa dini mbali mbali.

Papa Francis aliwasili Baghdad Ijumaa tarehe 5 Machi na kulakiwa na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi. Katika safari hiyo ya siku tatu kiongozi wa Kanisa Katoliki amekutana na Wakristo wa Iraq, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali ya nchi hiyo. Kabla ya safari hiyo Papa Francis alisema anataka kukutana na watu waliokumbana na mashaka mengi katika miaka ya hivi karibuni. 

342/