Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Machi 2021

08:08:33
1121323

Kiongozi Muadhamu: Harakati za mazingira ni harakati za kidini na kimapinduzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitia kuwa, harakati za mazingira ni harakati za kidini na kimapinduzi na haipasi kuzitazama kwa jicho la mapambo na vitu vya starehe.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Sayid Ali Khamenei amesema hayo leo Ijumaa hapa mjini Tehran wakati alipopanda miche miwili ya miti ya matunda katika bustani ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Maliasili na Siku ya Kupanda Miti nchini Iran na kueleza kwamba, majani na mazingira ya kijani kibichi ni sababu muhimu katika maisha na katika kutengeneza ustaarabu wa mwanadamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mizizi ya maarifa na dini katika kuyazingatia mazingira na kueleza kwamba,  kupanda mimea na miche ni miongoni mwa matendo na amali njema ambazo zimetiliwa mkazo katika sheria ya dini tukufu ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia umuhimu wa mazingira katika Katiba na kubainisha kwamba, kuweko mazingira tofauti ya kijiografia hapa nchini ni fursa mwafaka kwa ajili ya  vijana na wananchi kuwa na harakati amilifu katika uga wa mazingira.

Kiongozi Muadhamu ameonyesha kusikitishwa kwake na vitendo vya uharibifu wa misitu na maliasili kunakofanywa na watu wenye tamaa ya kufaidika na kusisitiza kwamba, kuharibu mazingira ni balaa kubwa ambayo inaharibu mustakabali wa mwanadamu, hivyo viongozi na wananchi wote kwa ujumla wanapaswa kusimama kidete na kukabiliana na vitendo hivyo.

Kadhalika Ayatullah Khamenei ameashiria matukio kama kuchomwa moto misitu, kukauka maziwa na ardhi zenye rutuba na kusisitiza kwamba, inawezekana kuzuia matukio haya yasitokee, na viongozi ambao hawatekelezi majukumu yao ndio wakosa na wenye hatia katika matukio haya.

342/