Main Title

source : parstoday
Jumamosi

13 Machi 2021

11:38:07
1122883

Corona Brazil, zaidi ya watu 2000 wafariki dunia katika kipindi cha siku moja

Nchi ya Brazil imegeuka kuwa kitovu cha vifo vya ugonjwa wa COVID-19 duniani baada ya zaidi ya watu 2000 kufariki dunia kwa ugonjwa huo katika kipindi cha siku moja. Shirika la Afya Duniani WHO limetahadharisha kuhusu wimbi jipya la ugonjwa huo katika eneo zima la Amerika ya Latini.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA : Baada ya kupita karibu mwaka mzima tangu WHO iutangaze ugonjwa wa COVID-19 kuwa ni janga la dunia, bado Brazil ina idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, suala ambalo limeitia wasiwasi mkubwa jamii ya kimataifa.

Waziri wa Afya wa Brazil ametangaza kuwa, watu 2,286 wamefariki dunia kwa corona katika kipindi cha masaa 24 nchini humo. Kesi mpya za ugonjwa huo zilizothibitishwa katika kipindi cha siku moja ni 79,876, na idadi hiyo ni rekodi ya pili kubwa ya maambukizi ya corona nchini humo tangu mwezi Februari 2020.

Marekani ndiyo inayoongoza dunia kwa rekodi ya vifo na wagonjwa wengi wa COVID-19. Hata hivyo katika kipindi cha wiki za hivi karibuni, takwimu zinazotolewa na serikali ya nchi hiyo zinaonesha kupungua kwa kiwango fulani vifo na maambukizo ya ugonjwa wa corona huko Marekani.

Tedros Adhanom, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO aliwasili nchini Brazil wiki iliyopita kwa ajili ya kuangalia kwa karibu hali halisi ya ugonjwa huo nchini humo. Alitahadharisha kwamba, hali mbaya ya ugonjwa wa corona nchini Brazil, ni hatari kubwa kwa eneo zima la Amerika ya Latini.

Wataalamu wa afya mbali na kuonya kuhusu kuzidiwa mahospitali ya Brazil na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona, wametahadharisha pia kwamba, ugonjwa wa COVID-19 nchini Brazil ni kama bomu la atomiki, unaweza kuleta madhara makubwa dunia nzima iwapo hautodhibitiwa.

342/