Main Title

source : parstoday
Jumamosi

13 Machi 2021

11:49:34
1122892

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika sikukuu ya Mab’ath; sisitizo la kusimama kidete Iran dhidi ya mfumo wa ubeberu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, malengo ya zawadi kubwa ya Mwenyezi ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW ni kuanzishwa utawala wa sheria za Mwenyezi Mungu, kuleta uadilifu na kupatikana maisha mazuri na yaliyo bora.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo jana katika hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Mab’ath na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW ambapo aliashiria pia kuendelea uadui dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kutokana na kupinga na kukataa kwake mfumo wa ubeberu na kusema kuwa, hii leo pia ambapo katika propaganda za kambi ya ubeberu, mfumo wa Kiislamu unajulikana kwa jina la Uislamu wa kisiasa umekuwa ukiandamwa na mawimbi ya kila aina ya hujuma na njama, na hiyo ni kwa sababu mfumo huu umeweza kuanzisha utawala wa sheria za Mwenyezi Mungu na kuwapatia wananchi wa taifa hili utambulisho wa kidini na Kiislamu.

Tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini, madola makubwa kibeberu na waingiliaji wa masuala ya ndani ya eneo la Asia Magharibi, walisimama na kuanzisha upinzani dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kwa njia hiyo waweze kuhuisha satwa na ubeberu wao.

Kwa mtazamo huo, hotuba ya Kiongozi Muadhamu ina nukta muhimu na za kistratejia ambazo kimsingi zinasisitiza juu ya mambo mawili muhimu.

Jambo la kwanza;  umuhimu wa kusimama kidete na kukabiliana na mashinikizo na vizingiti vigumu,msimamo ambao una umuhimu mkubwa katika harakati ya kusonga mbele na kuainisha mustakabali wenye hamasa zaidi. Kuhusiana na hili, Ayatullah Khamenei ameashiria juu ya kuendelea uadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu na kusisitiza kwamba, ili kukabiliana na adui amilifu na ambaye daima anapanga mbinu na kuandaa mikakakati kunahitaji mambo mawili muhimu ambayo ni “muono wa mbali” na “subira na kusimama kidete”.

Jambo la pili; ni sisitizo la kulinda mambo yanayopelekea kupatikana nguvu ya kweli ya taifa na kuwa macho mbele ya njama na madhara yanayoelekezwa dhidi ya mfumo na thamani pamoja na malengo ya mapinduzi. Taifa la Iran kwa kusimama kwake imara mbele ya watumiaji mabavu, limeupa changamoto mfumo wa kibeberu na harakati hii kubwa imepelekea kutokea mageuzi ya kimsingi  ambayo athari zake hii leo zinashuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi.

Matunda na mafanikio haya yanawezwa kuchunguzwa na kutathminiwa katika sehemu tatu za kukua Uislamu wa kisiasa, kuibuka mabadiliko katika kukigawa kipindi cha ukoloni na kuchomoza harakati za umma za kutaka mageuzi na mamlaka ya kujitawala na kuondokana na mfumo wa kibeberu katika eneo.

Sehemu nyingine ya hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu ilizungumzia  ujuba na undumakuwili wa madola ya Magharibi na upotoshaji wao wa mambo. Kuhusiana na hilo, Ayatullha Khamenei ameashiria masuala kama ya haki za binadamu, silaha za nyuklia, ugaidi na uwepo wenye uingiliaji wa kijeshi katika eneo na kusema kuwa, wananchi madhulumu wa Yemen kwa miaka sita sasa wamekuwa wakishambuliwa kwa mabomu na kukabiliwa na mzingiro wa kiuchumi, chakula na dawa kufuatia hujuma na vita vilivyoazishwa na utawala wenye roho mbaya na wa kidhalimu wa Saudi Arabia kwa himaya ya Marekani, na hakuna sauti yoyote ile ya kulalamikia hilo inayosikika kutoka katika asasi za kimataifa na katika madola ya Magharibi yanayodai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu.

Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, “kumiliki Marekani kiwanda kikubwa zaidi cha atomiki, kuuawa watu 220,000 kwa mabomu ya atomiki na wakati huo huo kudai kupingana na suala la silaha za maangamizi”, “hatua ya Washington ya kuuunga mkono utawala wa Saudi Arabia ambao unawaua wapinzani wake kwa kuwakatakata kwa msumeno na wakati huo huo kudai kwamba, ni mfuasi na mtetezi wa haki za binadamu” na kuanzisha na kuunga mkono makundi ya kigaidi kama Daesh na kuyapatia fedha, suhula za kisasa za vyombo vya habari sambamba na kuyaandalia mazingira ya kuuza mafuta ya Syria na wakati huo huo kudai kwamba, inaendesha vita dhidi ya ugaidi” ni mifano mingine ya wazi kabisa ya upotoshaji mambo unaofanywa na serikali ya Marekani.

Ukweli wa mambo ni kuwa, hii leo pia  mkabala na Iran kuna kambi kubwa ya dhulma, kufuru na ubeberu ambayo inafanya njama ikitumia kila wenzo, hila na suhula mbalimbali ili iulazimishe mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulegeze kamba na hatimaye usalimu amri.

Hapana shaka kuwa, hadi sasa taifa la Iran limeweza kuvuka vizingiti vingi vigumu kwa kushikamana na subira na kuwa na muono wa mbali na jambo lisilo na shaka ni kuwa, baada ya hapa pia litaweza kusimama kidete na kushinda matatizo yote yaliyoko mbele yake.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa na misingi yake ya kistratejia daima imekuwa ikifuatilia suala la amani na usalama na siku zote limekuwa katika mkondo wa kupigania uadilifu. Njia hii malengo yake yako wazi kabisa na hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imeonyesha njia sahihi ya harakati ya taifa la Iran kuelekea mustakabali wenye uhakika, ambao msingi wake ni mamlaka ya kujitawala na kutegemea nguvu na uwezo wa ndani na wakati huo huo, kuwa macho mkabala wa siasa za hadaa na hila za maadui.

342/