Main Title

source : parstoday
Jumatatu

24 Mei 2021

12:47:39
1143866

Watu wasiopungua 15 wafariki dunia, mamia ya nyumba yateketea, volcano ya Goma

Watu karibu 15 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana mlipuko wa volkano uliotokea katika Mlima wa Nyiragongo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Inaripotiwa kuwa yumkini idadi ya vifo ikaongezeka wakati maafisa wa serikali wakiendeleza juhudi za uokoaji katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Jumamosi iliyopita volkano ya Mlima Nyiragongo ililipuka na kumwaga ujiuji wa moto yaani lava uliolifanya anga kuwa jekundu, lakini lava hiyo haikufika katika mji wa Goma ulioko kusini mwa mlima huo unaokaliwa na watu milioni mbili.

Wakazi wa vijiji vya karibu na mlima huo pamoja na mji Goma ambao waliyakimbia makaazi yao kwa hofu ya mlipuko huo wameanza kurejea huku wengi wao wakiwasaka jamaa zao waliopotea.

Watu tisa miongoni mwa waliothibitishwa kufariki dunia, walipoteza maisha katika ajali za barabarani wakati watu walipokuwa wakihaha kukimbia ili kuokoa maisha yao.

Wanne walikufa walipokuwa wakijaribu kutoroka gerezani huku wawili wakiungua hadi kufa, alisema msemaji wa serikali, Patrick Muyaya Jumapili.

Zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kupotea na wengine 150 wametengana na familia zao, kulinga na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) ambalo linasema litaweka vituo vya kuwapokea watoto watakaopatikana wakiwa peke yao.

Mitikisiko ilisikika baada ya kulipuka kwa volkano hiyo, alisema Bw Muyaya. Wakazi wa Goma wameshauriwa kuendelea kuwa macho, kuepuka safari zisizo za lazima, na kufuata maelekezo yanayotolewa na maafisa husika..

Mlima huo wa volkano uliopo kilomita 10 (maili sita) kutoka Goma, ulilipuka mara ya mwisho mwaka 2002 na kusababisha vifo vya watu 250 huku watu wengine 120,000 wakiachwa bila makazi.

Wakazi wa Goma walianza kuzikimbia nyumba zao kabla ya serikali kutangaza mpango wa namna ya kuondoka katika mji huo.

Umati wa watu ulionekana usiku ukiondoka kwa miguu huku baadhi yao wakiwa wamebeba magodoro na mali zao nyingine

342/