Main Title

source : parstoday
Jumamosi

3 Julai 2021

11:47:13
1156314

Kuakhirishwa kesi ya Sheikh Zakzaky na njama za mabeberu nchini Nigeria

Mahakama ya Nigeria kwa mara nyingine tena imeakhirisha kikao cha kusikilizwa kesi ya kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky hadi tarehe 28 Julai licha ya Waislamu wa nchi hiyo kutaka mwanazuoni huyo aachiwe huru.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mahakama Kuu ya Jimbo la Kuduna imetangaza kuwa, imechukua uamuzi huo ili kutoa fursa ya kuchukuliwa maamuzi kuhusu faili hilo na kwamba, faili lenyewe lilikuwa bado halijafikishwa kwenye mahakama hiyo. Hata hivyo mshauri wa Sheikh Zakzaky amekadhibisha madai hayo akisema faili la kesi yake lilikuwa tayari limekabidhiwa mahakamani. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake, Mallimah Zeenah walitiwa nguvuni tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na amekuwa mahabusu kwa kipindi chote cha miaka 6 iliyopita. Mahakama ya Kaduna imekuwa ikikataa ama kumhukumu au kumuachia huru, na mara zote inatoa visingizio vya aina mbalimbali vya kuhalalisha kuendelea kumshikilia mahabusu. 

Sheikh Zakzaky anasumbuliwa na hali mbaya ya afya na anahitajia uangalizi maalumu wa madaktari. Hali mbaya ya kiafya ya mwanazuoni huyo imeshadidi zaidi kutokana na wimbi la sasa la maambukizi ya virusi vya corona. Siku chache zilizopita pia ilifichuliwa kwamba, maafisa wa gereza anakoshikiliwa walitaka kumuingiza mtu anayesumbuliwa na maradhi ya COVID-19 mahali alipo Sheikh Zakzaky, suala amblo lilipingwa vikali na mahabusu wenzake.

Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria hususan wafuasi wa madhehebu ya Ahlulbait yameongezeka sana hususan baada ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya IMN. Mikusanyiko ya kidini ya wafuasi wa kiongozi huyo imepigwa marufuku, na askari usalama wanakabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano au mkusanyiko wowote wa Waislamu hao. Kwa maneno mengine ni kuwa, serikali ya Abuja imefanya jitihada za kuwazuia kabisa Waislamu kushiriki katika harakai zote za kisiasa na kijamii nchini humo. 

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, sababu ya hatua hiyo ya serikali ya Abuja ni mabadiliko yaliyotokea katika siasa za kimataifa, utajiri wa Nigeria na nafasi yake katika masuala ya kimataifa. 

Nigeria inasifika kwa kuwa na utajiri wa mafuta na gesi na jamii kubwa ya watu ambavyo vinaifanya kuwa mojawapo ya nchi kubwa na muhimu za Afrika. Kwa msingi huo, baada ya Marekani, utawala wa kizayuni wa Israel na Saudi Arabia kufeli katika siasa zao kwenye eneo la Magharibi mwa Asia, tawala hizo zilianzisha jitihada za kupanua satua na ushawishi wao katika nchi nyingine hususan barani Afrika; hivyo waliilenga Nigeria kupitia njia ya kuwashawishi maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo. Is’haq Adam ambaye ni wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky anasema: Marekani, Israel na Saudi Arabia wamempa Muhammadu Buhari jukumu la kukabiliana na hata kummaliza kabisa kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria, na katika uwanja huu Saudia imetoa mamilioni ya dola kwa maafisa wa serikali ili kukamilisha lengo hilo.

Sheikh Adam Ahmad ambaye ni mjumbe wa Sheikh Ibrahim Zakzaky ameashiria ripoti inayoonesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa na nafasi kubwa katika kuzidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria na katika kurefusha kesi ya msomi huyo wa Kiislamu na kusema: Mbali na mashinikizo ya Israel kwa serikali ya Abuja, serikali za Marekani na Saudia pia zinakwamisha mchakato wa kushughulikiwa kesi ya Sheikh Zakzaky na mkewe.

Pamoja na hayo yote, Waislamu wa Nigeria wameendelea kusimama imara kwa ajili ya kumtetea kiongozi wao kwa kutumia majukwaa na minasaba mbalimbali. Waislamu hao wamekuwa wakiandamana kila mara na kutumia majukwaa ya kitaifa na kimataifa kuwakumbusha walimwengu dhulma na manyanyaso yanayompata Sheikh Zakzaky na mkewe, Mallimah Zeenah wanaoshikiliwa mahabusu kwa miaka kadhaa sasa bila sababu yoyote ya maana.

Mhadhiri wa chuo kikuu nchini Nigeria, Umar Zaky anasema: “Serikali ya Abuja inashirikiana kwa karibu na Saudi Arabia kwa ajili ya kuwakandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia na kufuta kabisa satua na ushawishi mkubwa wa Sheikh Zakzaky. Tawala hizi mbili pia zinafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, habari zote zinazohusiana na Sheikh Zakzaky zinazuiliwa kabisa.”

Alaa kulli hal, japokuwa serikali ya Nigeria imefanikiwa tena kuakhirisha zoezi la kusikilizwa kesi ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu lakini wafuasi wake wameapa kwamba, hawatatulia hadi pale kiongozi huyo atakapoachiwa huru.

342/