Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

26 Mei 2022

12:16:05
1261197

Vitoto vichanga 11 vyatekeketea kwa moto hospitalini nchini Senegal

Watoto wachanga 11 wamefariki dunia katika ajali ya moto iliyotokea kwenye hospitali moja ya mji wa Tivaouane wa magharibi mwa Senegal.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Jana Jumatano usiku kwa wakati wa Senegal Rais Macky Sall wa nchi hiyo alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuelezea kusikitishwa mno na tukio hilo.

"Nimepokea kwa uchungu na kufadhaika, taarifa ya vifo vya watoto 11 wachanga vilivyotokea kwenye ajali ya moto katika kitengo cha watoto wachanga cha hospitali ya umma. Ninawapa mkono wa pole na wa masikitiko makubwa mama wa watoto hao na familia zao," ameandika Rais Sall kwenye ujumbe wake huo wa Twitter.

Mamlaka za hospitali hiyo zimesema kuwa, moto huo umesababishwa na matatizo ya umeme. Ni watoto watatu pekee ndio waliookolewa kwenye ajali hiyo ya kusikitisha.

Waziri wa Afya wa Senegal, Abdoulaye Diouf Sarr, ambaye yuko Geneva kushiriki katika kikao cha Mawaziri wa Afya Ulimwenguni, amesema atakatisha safari hiyo na kurejea Senegal mara moja.

Demba Diop Sy, Meya wa Tivaouane, ambao ni moja ya miji muhimu sana ya Senegal na ni kitovu cha usafiri, amesema kuwa, polisi na kikosi cha zimamoto bado walikuweko hospitalini wakati anatoa taarifa hiyo, lakini hakutoa maelezo zaidi.

Tukio kama hilo lilitokea katika mji wa kaskazini wa Linguere mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, wakati moto ulipozuka hospitalini na kupelekea watoto wanne wachanga kupoteza maisha yao.

342/