Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

26 Mei 2022

12:16:43
1261198

Afrika imehusika kidogo mno na uchafu wa mazingira, lakini ndiyo inayoathirika zaidi duniani

Uchunguzi mpya uliofanywa na Mo Ibrahim unaonesha kuwa, nchi zote za bara la Afrika, zimechangia kwa asilimia 3.3 tu ya uzalishaji wa gesi chafu na uchafuzi wa mazingira duniani tangu mwaka 1960, lakini pamoja na hayo, nchi za bara hilo ndizo zinazoathiriwa zaidi mabadiliko ya tabianchi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa, kuna wajibu wa kuzingatiwa kwa sura ya kipekee bara la Afrika katika mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Watu walioathiriwa vibaya na ukame katika miaka ya baina ya 2010 hadi 2022 hawapungui milioni 172.3 huku wale waliopata hasara kutokana na mafuriko wakiwa hawapungui milioni 43.0

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waathiriwa wakubwa wa uchafuzi wa mazingira duniani ni nchi za Afrika ambapo asilimia 20.1 ya wakazi wa bara hilo ni wahanga wa uchafuzi huo. Uchunguzi unaonesha kuwa, ifikapo mwaka 2030, wakazi wengi wa nchi za chini ya jangwa la Sahara barani Afrika watatumbukia kwenye ukata na umaskini wa kupindukia kutokana na uchafunzi wa hali ya hewa unaofanywa na nchi za mabara mengine.

Ripoti hiyo ya kuhusika kwa kiwango kidogo mno bara la Afrika katika uchafuzi wa mazingira licha ya kwamba madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanazitesa zaidi nchi za Afrika imetolewa katika hali ambayo, sherehe za maadhimisho ya Siku ya Afrika zilifanyika kote duniani jana Jumatano huku kilele cha sherehe hizo kikiwa ni mkutano usio wa kawaida wa viongozi wa Afrika unaofanyika, Malabo, Guinea ya Ikweta (Equatorial Guinea).

Siku ya Afrika huadhimishwa kila mwaka mnamo Mei 25 kwa mnasaba wa kutiwa saini Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) miaka 59 iliyopita huko Addis Ababa Ethiopia. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) na hivi sasa umoja huo una wanachama 55.

AU mwaka huu inaadhimisha mwaka wa 20 tokea kuanzishwa kwake na kumewekwa ratiba maalumu za kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu.

342/