Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

28 Mei 2022

12:53:22
1261691

Wasiwasi wa UN kuhusu ongezeko la wakimbizi DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu mahitaji ya dharura na makubwa ya zaidi ya watu 72,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano katika siku za hivi karibuni katika Jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Katika taarifa Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amesema, “Tangu tarehe 19 Mei, mapigano makali yametikisa maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo huku wanamgambo wanaodai kuwa sehemu ya kundi lenye silaha la M-23 wakipambana na vikosi vya serikali katika mapambano yanayoendelea kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa jimbo hilo.” 

Takriban raia 170,000 wameyakimbia makazi yao tangu kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC kuanzia Novemba 2021. Wimbi la hivi karibuni la ghasia limesababisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao kutafuta usalama katika maeneo tofauti ya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na Goma. Katika wiki iliyopita pekee, watu takriban 7,000 pia wameripotiwa kuvuka hadi nchi jirani ya Uganda nchi ambayo tayari inawahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1.5. 

Bi Matoo ameendelea kueleza hali ilivyo akisema, “Wale wanaohama, njiani wanakabiliwa na vurugu za mara kwa mara. Mashamba na maduka yameachwa katika hatari kubwa ya kuporwa, hivyo kutishia maisha. Wanawake na wasichana wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji, pamoja na vitisho vya kimwili na unyang'anyi wa pande zinazozozana.”  

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wakimbizi wa ndani, IDPs, wapatao milioni 5.6, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa na idadi kubwa zaidi ya ukimbizi wa ndani barani Afrika.

342/