Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

30 Mei 2022

13:53:20
1262318

Rais wa Russia azionya nchi za Magharibi kuhusu kuipa Ukraine silaha

Rais wa Russia Vladimir Putin amewaonya vikali viongozi wa Ujerumani na Ufaransa kuhusu kupeleka msaada wa silaha nchini Ukraine, akisema hatua hiyo inaweza kuvuruga zaidi utulivu katika nchi hiyo.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Kwa mujibu wa Ikulu ya Kremlin, Putin ametoa kauli hiyo katika mazungumzo ya simu na  Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani kuwa kuendelea kuipatia Ukraine silaha ni "hatari", akionya juu ya hatari ya kuongezeka mzozo wa kibinadamu.

Aidha amesema kuendelea kuipa Ukraine silaha kuna maana ya kurefushwa zaidi vita.

Katika mazungumzo na viongozi hao wawili jana Jumamosi, Putin amesema pia Russia iko tayari kujadili juu ya njia za kuiwezesha tena Ukraine kusafirisha nafaka kutoka bandari ya Bahari Nyeusi. Putin amesisitiza kuwa ukosefu wa chakula duniani ambao umepelekea bei kupanda umesababishwa na sera potovu za nchi za Magharibi ambazo zimeiwekea Russia vikwazo.

Russia na Ukraine ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa ngano na mafuta ya kupikia duniani, huku Russia ikiwa pia muuzaji muhimu wa mbolea katika soko la kimataifa. Kremlin imeongeza kuwa, Putin alimjulisha Macron na Scholz kuwa Russia iko tayari kuongeza mauzo ya nje ya mbolea na bidhaa nyingine za kilimo iwapo tu vikwazo dhidi yake vitaondolewa- ombi ambalo amelitoa pia katika mazungumzo yake na viongozi wa Italia na Austria katika siku za hivi karibuni.

342/