Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

26 Agosti 2022

10:49:08
1300800

Kuongezeka mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya

Licha ya nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza, kuweka sheria kali za kuzuia kuingia wahajiri, lakini idadi ya wahajiri hao imeongezeka bali hata hivi sasa imevunja rekodi ya kuingia nchini Uingereza tena kupitia kanali ile ile ya baharini ya English Channel.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, Jumatatu wiki hii, wahajiri 295 walifanikiwa kuingia nchini humo kwa njia boti zinazofanya magendo. Rekodi ya huko nyuma ilikuwa ni ile ya tarehe 11 Novemba 2021 ambapo wahajiri 185 walifanikiwa kuingia nchini Uingereza katika kipindi cha masaa 24. Takwimu mpya za serikali ya Uingereza zinaonesha kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, wakimbizi 22,670 wameingia nchini humo kimagendo kwa kutumia boti wakitokea kaskazini mwa Ufaransa. Hii ni katika hali ambayo mwaka jana na katika kipindi kama hiki, wakimbizi 11,300 ndio walifanikiwa kuvuka mfereji wa English Channel na kuingia Uingereza kimagando. Rekodi hiyo mpya ya wakimbizi wanaoingia Uingereza kimagendo imevunjwa katika hali ambayo serikali ya London imeweka sheria kali na kandamizi za kukabiliana na wakimbizi hao. Uingereza hata imefikia makubalaiano na Rwanda ya kuwahamishia nchini humo wakimbizi hao, lakini wimbi lake limeongezeka na kuvunja rekodi badala ya kupungua. 

English Channel ni mfereji wa baharini unazitenganisha Uingereza na Ufaransa na ni moja ya njia zinazopita vyombo vingi vya baharini duniani. Lakini katika kipindi cha wiki za hivi karibuni cha kuongezeka wimbi la wahajiri haramu wanaoingia kimagendo nchini Uingereza kutokana na migogoro mingi kama ule wa Ukraine, ukame na hali mbaya za maisha katika nchi mbalimbali duniani, magendo ya binadamu nayo yameongezeka na wengi wao wanatumia njia hiyo kuingia Uingereza. Licha ya serikali ya London kuweka sheria kali na vizuizi vingi lakini wahajiri hao wako tayari kuhatarisha maisha yao, kutumia boti mbovu na zisizo salama kuingia barani Ulaya kwa gharama ya hata roho zao na za watoto wao. Cha kusikitisha zaidi ni kuwa, mara kwa mara kumekuwa kukiripoti taarifa za kutisha za kuzama na kufa maji wahajiri wengi wanaojaribu kuelekea barani Ulaya. 

Mwezi Novemba mwaka jana kulitokea ajali ya kutisha mno ambayo haijawahi kutokea mfano wake katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kwenye English Channel. Jahazi moja linalotumia tanga, lilipinduka na kuzama kwenye mfereji huo wakati lilipokuwa linaelekea nchini UIngereza na kusababisha vifo vya wote waliokuwemo. Miili ya wahajiri 27 iliokotwa ikiwa imegugutaa kwa baridi katika fukwe za Ufaransa.

Kiujumla tunaweza kusema kuwa, moja ya malengo ya wahafidhina wa Uingereza ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya ni kutaka wapate fursa ya kufanya ukandamizaji wowote wanaotaka dhidi ya wahajiri wanaoingia nchini humo. Viongozi hao wameonesha wazi kuwa hawashughulishwi na misingi ya haki za binadamu katika ukandamizaji wao huo. Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, Priti Patel, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza  alitangaza mkataba uliolalamikiwa mno wa pound milioni 120 wa kuhamishiwa nchini Rwanda, wahajiri wote wanaoingia kimagendo huko Uingereza. Hatua hiyo ililaumiwa vikali na taasisi za haki za binadamu pamoja na Umoja wa Mataifa lakini viongozi wahafidhina wa Uingereza waliendelea kushikilia msimamo huo wa kuwahamishia Rwanda, wahajiri wanaoingia kinyume cha sheria nchini humo.

342/