Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Agosti 2022

17:18:00
1301227

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yasikitishwa na machafuko mapya ya Libya

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameelezea kusikitishwa sana na machafuko mapya ya nchini Libya na ametaka kukomeshwa mara moja mapigano hayo. Amesema, Tehran inazitaka pande hasimu kuzingatia maslahi ya taifa, usalama wa wananchi na kutatua mambo yao kwa njia ya mazungumzo.

Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo Jumapili na huku akielezea kusikitishwa kwake na mapigano ya mjini Tripoli Libya amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazitaka pande zote hasimu kuvumiliana na kujizuia kuwasha moto zaidi wa mapingano na badala yake wazingatie zaidi maslahi ya kitaifa ya wananchi wa Libya.

Takwimu za duru za tiba nchini Libya zinaonesha kuwa watu wasiopungua 23 wameuawa na kwa uchache 87 wamejeruhiwa katika mapigano makali yaliyozuka upya Jumamosi asubuhi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Vikosi vya jeshi vimesambazwa mjini Tripoli kufuatia kushadidi mzozo wa kisiasa kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa GNU inayoongozwa na Waziri Mkuu wake Abdul Hamid Al-Dabibah na serikali iliyopewa mamlaka na bunge lenye makao yake mjini Tabruk mashariki ya nchi ambayo inaongozwa na Fathi Bashagha.

Taarifa iliyotolewa na mrengo wa GNU imesema mapigano hayo mapya yaliyozuka mjini Tripoli yalichochewa na hatua ya wapiganaji watiifu kwa mrengo wa Bashagha kuufyatulia risasi msafara wa askari wa GNU.

Mapigano hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi kutokea kwa muda wa miaka miwili sasa mjini humo na yanahofiwa kusababisha vita vingine vya nchi nzima.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, meya wa mji mkuu wa Libya amesema hali ni ya maafa katika maeneo kadhaa ya Tripoli, na akafafanua kwamba, mapigano katika mji huu bado yanaendelea. Chuo kikuu cha Tripoli kimetangaza kusitishwa masomo na mitihani kutokana na mapigano hayo.

342/