Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Agosti 2022

17:19:19
1301230

Iran na Nigeria kupanua ushirikiano wao katika uga wa nishati

Waziri wa Mafuta wa Iran ameeleza matumaini yake ya kuimarika ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Nigeria katika uga wa nishati.

Javad Owji, Waziri wa Mafuta wa Iran alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake na Waziri wa Rasilimali za Petroli wa Nigeria, Timipre Sylva, pambizoni mwa mkutano wa Jukwaa la Nchi Zinazouza Nje Gesi (GECF).

Owji amesema Iran na Nigeria zina uwezo mkubwa katika sekta ya nishati, na kwamba nchi mbili hizi zina fursa ya kuimarisha ushirikiano wao katika uga huo, baada ya pande mbili kusaini Mikataba ya Maelewano.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nigeria zina hifadhi kubwa za mafuta na gesi, huku Nigeria ikiwa muuza mkubwa wa sita wa gesi ya LNG duniani.

Waziri wa Mafuta wa Iran amesisitiza kuwa, "Tumesaini Mikataba ya Maelewano ya kupanua ushirikiano katika uga wa mafuta, gesi na petrokemikali, na upelekaji nje huduma za kiufundi na kiuhandisi, na vile vile ustawi wa nishati."

Kwa upande wake, Waziri wa Rasilimali za Petroli wa Nigeria, Timipre Sylva amesema imeafikiwa kuwa Iran itatuma teknolojia ya CNG nchini Nigeria, na mkabala wake itastafidi na teknolojia ya Nigeria ya LNG.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa mapatano baina ya Tehran na Abuja, ukarabati wa kampuni za kusafisha mafuta za Nigeria utafanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/