Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

2 Septemba 2022

14:45:33
1302692

Kadhaa wauawa katika mapigano mapya ya kikabila Blue Nile, Sudan

Kwa akali watu saba wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyozuka katika jimbo la Blue Nile, kusini mwa Sudan.

Kamati ya usalama ya jimbo hilo imesema katika taarifa kuwa, inachunguza chimbuko la mapigano hayo yaliyojeruhi watu 23, na ambayo yamejiri wiki chache baada ya mapigano makali ya umwagaji damu kushuhudiwa katika eneo hilo.

Kamati hiyo imetoa agizo la kutotoka nje nyakati za usiku katika miji miwili mikubwa ya jimbo hilo, sanjari na kupiga marufuku mikusanyiko yoyote au maandamano.

Katikati ya mwezi Julai mwaka huu, watu 105 waliuawa, huku maelfu ya wengine wakiachwa bila makazi katika mapigano mengine ya kikabila baina ya jamii za Hausa na Funj katika jimbo hilo.

Wataalamu wanasema mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana, yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, yalizua ombwe la usalama ambalo limechochea kuibuka tena kwa ghasia za kikabila, katika nchi ambayo mapigano makali yanazuka mara kwa mara kuhusu ardhi, mifugo, upatikanaji wa maji na malisho.

Mnamo Aprili, mapigano mengine ya kikabila yalipelekea kuuawa zaidi ya watu 200 katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan, ambalo hushudia vita na mapigano mara kwa mara.

342/