Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

3 Septemba 2022

20:22:40
1303044

UNESCO: Mamilioni ya watoto hawaendi shule licha ya kuanza msimu wa masomo

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetangaza kuwa, mamilioni ya watoto hawaendi shule katika maeneo mbalimbali ya dunia licha ya kuanza msimu mpya wa masomo.

Wakati msimu mpya wa masomo ukianza sehemu mbalimbali duniani, takwimu mpya zilizotolewa na shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) zinaonyesha kwamba, watoto na vijana milioni 244 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 18 duniani kote bado hawaendi shule.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zinasalia kuwa ukanda wenye watoto wengi zaidi wasioendfa shuleni ambao ni milioni 98 na pia ndio ukanda pekee ambako idadi inaongezeka.

Ukanda wa Kati na Kusini mwa Asia unashikilia nafasi ya pili ya idadi kubwa ya watoto ambao hawako shuleni, ambayo ni milioni 85. 

Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), ametoa mwito kuchukuliwa hatua za pamoja ili kuhakikisha kwamba haki ya kila mtoto kupata fursa ya elimu bora inaheshimiwa.

Ametahadharisha kwamba "Kwa kuzingatia matokeo haya, lengo la elimu bora kwa wote ifikapo mwaka 2030, lililowekwa na Umoja wa Mataifa, lina hatari ya kutofikiwa. Tunahitaji uhamasishaji wa kimataifa ili kuweka elimu katika kipaumbele cha ajenda ya kimataifa."

342/