Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Septemba 2022

18:28:07
1303335

Magaidi wa al Shabab waua raia wasiopungua 18 na kuchoma moto malori ya chakula katikati ya Somalia

Genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab limeua raia wasiopungua 18 katika eneo la Hiran la katikati mwa Somalia na kuteketeza kwa moto malori yaliyokuwa yamesheheni chakula kwa ajili ya watu wenye njaa wa eneo hilo.

Genge hilo lenye silaha lilianzisha mashambulizi katika eneo la Hiran katika jimbo la Hirshabelle la katikati mwa Somalia wakati malori yaliyokuwa yakisafirisha chakula kutoka mji wa Baladweyne kuelekea katika mji wa Mahas, yalipokuwa yanapita kwenye eneo hilo. 

Farah Adem, mzee mmoja wa eneo hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema: "Al-Shabab wameua raia 18 na kuchoma moto malori kadhaa ya chakula cha msaada yaliyokuwa yakielekea katika mji wa Mahas jana usiku." 

Shirika la habari la serikali ya Somalia SONNA nalo limeripoti kwamba magaidi wa al-Shabab wamechoma moto malori na kuua watu wengi waliokuwa kwenye magari hayo. 

Mzee Aden amesema wakaazi wenye silaha wa eneo hilo waliwafurusha magaidi hao wiki iliyopita lakini serikali haikutuma wanajeshi kusaidia kuzuia kurejea magaidi hao wakufurishaji.

“Al-Shabab wanafanya mambo haya yote ili kutulazimisha tujisalimishe. Lakini hatutasalimu amri kwa al-Shabab mradi tu kuna roho ndani yetu. Vikosi vya serikali bado havijafika eneo letu,” amesema mzee Farah Aden.

Mara kwa mara genge la al Shabab hufanya mashambulizi ya mabomu, ya bunduki na mashambulizi mengineyo dhidi ya askari usalama na raia.

Mwezi uliopita wa Agosti, zaidi ya watu 20 waliuawa katika shambulio lililofanywa na magaidi wa al-Shabab wakati walipovamia Hoteli ya Hayat mjini Mogadishu. Baada ya uvamizi huo kulizuka mapigano ya saa 30 wakati wanajeshi wa serikali walipoendesha operesheni ya kuvunja jaribio hilo la magaidi wa al shabab na kuwaachilia huru mateka.

342/