Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

5 Septemba 2022

16:04:15
1303676

Ujumbe wa Israel wafanya safari ya kificho nchini Misri

Ujumbe wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya safari ya siri nchini Misri kwa lengo la kujaribu kupunguza taharuki baina ya Cairo na Tel Aviv.

Shirika la al-Araby al-Jadeed limenukuu ripoti ya radio inayosimamiwa na jeshi la utawala wa Kizayuni ikisema kuwa, ujumbe huo wa Wazayuni nchini Misri uliongozwa na Avi Gil, katibu wa masuala ya kijeshi wa Yair Lapid, Waziri Mkuu wa Israel.

Habari zaidi zinasema kuwa, ujumbe huo wa Kizayuni umekukata na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Misri, na kuzungumzia mzozo ulioibuka baina ya Tel Aviv na Cairo.

Inaarifiwa kuwa, moja ya mambo yaliyochangia kuingia doa uhusiano wa pande mbili hizo ni mashambulizi ya anga ya jeshi katili la utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Agosti 5.

Makumi ya Wapalestina wakiwemo watoto 17 na makamanda wa harakati ya Jihadul Islamu waliuawa shahidi katika hujuma hizo za Wazayuni Gaza.

Hii ni katika hali ambayo, wanaharakati wa Misri wamekuwa wakionya kuwa, hatua ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kujipendekeza kwa utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yao ni tatizo kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu.

342/