Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

8 Septemba 2022

11:18:50
1304651

Kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa yatupiliwa mbali

Majaji nchini Ufaransa wametupilia mbali kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda iliyokuwa ikiwakabili wanajeshi wa nchi hiyo.

Majaji hao wanasema kuwa, hakuna ushahidi kwamba wanajeshi wa Ufaransa walihusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka wa 1994 nchini Rwanda.

Waendesha mashtaka walianzisha uchunguzi wa uhalifu dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Ufaransa waliopelekwa Rwanda na kutuhumiwa kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Lakini majaji wanaosimamia kesi hiyo wameamua kutoendelea na kesi dhidi ya wanajeshi hao wakieleza kwamba, hakuna ushahidi wa kutosha. 

Pia hawakupata ushahidi wa ushiriki wa vikosi vya Ufaransa katika mauaji yaliyofanywa kwenye kambi za wakimbizi au kwamba wanajeshi hao waliwasaidia Wahutu.

Ufaransa kwa miongo mingi imekabiliwa na tuhuma za kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari ya Rwanda. Mwaka jana, Rais Emmanuel Macron aliwaomba Wanyarwanda kuisamehe Ufaransa kwa jukumu lake katika mauaji hayo.

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokea kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Shambulizi hilo lilipelekea wanajeshi wa Kihutu wa serikali na wanamgambo waitifaki waliokuwa na misimamo mikali kuanzisha mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwaangamiza Watutsi waliokuwa wachache ambapo watu 800,000 waliuawa katika mauaji hayo.

342/