Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

8 Septemba 2022

11:24:19
1304660

Mazungumzo ya kitaifa ya Chad yaongezewa muda; kuendelea hadi Septemba 30

Mazungumzo ya kitaifa ya Chad yaliyoanzishwa na kundi la jeshi linalotawala nchini humo yameongezwa muda wake baada ya kuibuka changamoto kadhaa.

Taarifa zaidi zinasema, mazungumzo hayo ya amani muda wake umeongezwa  kwa siku 10 zaidi baada ya kuvurugika mara kadhaa.

Mjadala huo wa kitaifa unaohusisha makundi mbali mbali kwa lengo la kurejesha utawala wa kiraia ulianza mwezi uliopita, ukipangwa kumalizika Septemba 20. Tarehe ya mwisho sasa imesogezwa hadi Septemba 30.

Zaidi ya wajumbe 1,400 kutoka utawala wa kijeshi, mashirika ya kiraia na baadhi ya wanasiasa wa upinzani pamoja na muungano wa vyama vya wafanyakazi, wamekuwa jijini N'Djamena mji mkuu wa Chad kwa ajili ya kushiriki kwenye mazungumzo hayo ya amani.

Mazungumzo hayo yameahirishwa mara kadhaa hapo kabla kutokana na sababu mbalimbali hasa baada ya makundi yenye silaha pamoja na makundi ya upinzani kususia, yakidai kwamba mazungumzo hayo ni kati ya serikali na washirika wake wa karibu.

Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno anaongoza baraza la kijeshi lenye wajumbe 15, baada ya kuchukua madaraka, kufuatia kifo cha baba yake wakati akiwa kwenye uwanja wa vita dhidi ya waasi Aprili 2021.

Kiongozi huyo amebuni mjadala wa kitaifa kwa nia ya kuitisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia katika kipindi cha miezi 18. Kikao hicho hicho kufikia sasa hakijapiga hatua kubwa kuelekea kwenye malengo yake.

342/