Main Title

source : Parstoday
Jumatano

21 Septemba 2022

17:01:14
1307031

OIC yatahadharisha kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Hissein Brahim Taha ameelezea wasiwasi wa jumuiya hiyo kuhusiana na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu katika baadhi ya nchi za Ulaya.

Kikundi cha Mawasiliano kuhusu Waislamu barani Ulaya cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kimefanya mkutano wa wazi mjini New York, kando ya Kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ukiongozwa na Katibu Mkuu wa OIC, mkutano huo ulifanyika kwa ombi la serikali ya Uturuki. Katibu Mkuu wa OIC, Hissein BrahimTaha, katika taarifa yake ameeleza wasi wasi wa OIC kuhusiana na kukithiri kwa chuki dhidi ya Uislamu katika baadhi ya nchi za Ulaya na kutoa wito wa kufanyika juhudi zaidi za kuimarisha ushirikishwaji na mazungumzo ili kukuza maelewano baina ya tamaduni , kustahamiliana na kuheshimiana.

Mkutano huo ulitathmini hali ya jumla ya Waislamu barani Ulaya tangu mkutano wa mwisho wa Kikundi cha Mawasiliano, uliofanyika tarehe 22 Machi 2022 mjini Islamabad.

Mkutano huo umeeleza wasi wasi wake mkubwa juu ya ongezeko la kutia hofu la chuki dhidi ya Waislamu, chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia, matamshi ya chuki na misimamo mikali ya mrengo wa kulia na mwenendo wa matukio ya ukatili dhidi ya Waislamu katika baadhi ya nchi za Ulaya unaochochewa na matamshi ya chuki na ubaguzi ulioenea.

Katika matamshi yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistani Bilawal Bhutto Zardari alisisitiza kwamba chuki dhidi ya Uislamu - ambayo ina mizizi katika historia ya Ulaya - sasa imekuwa janga katika nchi kadhaa ulimwenguni, na kuongeza kuwa imedhihirika vibaya zaidi nchini India. Alibainisha kuwa ongezeko la uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu pamoja na ubaguzi katika elimu, uraia, uhamiaji, ajira, nyumba na huduma za afya, miongoni mwa mengine, ni kumbukumbu za kutosha. Aidha amesema chuki hiyo imechukua pia mwelekeo wa kijinsia ambao  wasichana na wanawake wa Kiislamu wanalengwa kutokana na mtindo wa mavazi yao.

Amewasilisha mpango wenye vipengele vinne kwa ajili ya ulinzi bora wa Waislamu walio wachache barani Ulaya na kuzitaka nchi wanachama wa OIC, ndani ya fremu ya uhusiano wao wa pande mbili na nchi za Ulaya, kuibua changamoto zinazowakabili Waislamu barani Ulaya na kufanya jitihada mahususi za kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.

342/