Main Title

source : Parstoday
Jumatano

21 Septemba 2022

17:04:28
1307037

Mkutano wa UNGA: Rais Tshisekedi aituhumu Rwanda kuivamia DRC

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameituhumu Rwanda hadharani kwamba, imevamia ardhi ya nchi yake.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kueleza kwamba, licha ya nia njema ya serikali yake na mkono wa amani ulionyooshwa na raia wa DRC, lakini shukurani ya baadhi ya majirani imekuwa kuunga mkono makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tshisekedi ameitaja kwa jina Rwanda, akidai iliwaingiza wanajeshi wake ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi Machi, kwa kukiuka sheria za kimataifa na mkataba wa Umoja wa Mataifa. Aidha, rais Tshisekedi ameituhumu Rwanda kwamba, inawasaidia waasi wa M23 katika kuiangusha helikopta ya walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, tukio lililosababisha vifo wa watu wanane.Ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo duru za habari imeona nakala yake, ilisema jeshi la Rwanda liliingilia kati dhidi ya ngome za jeshi la Kongo kuanzia Novemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu.

Mwezi uliopita Rwanda ilipuuzilia mbali madai kwamba jeshi lake liliunga mkono waasi wa M23 kushambulia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo; madai yaliyomo katika ripoti ya Kundi la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Kumekuweko mvutano wa miezi kadhaa kati ya DRC na Rwanda kuhusu shughuli za waasi, huku Kinshasa ikiituhumu mara kwa mara Rwanda kuwa inaunga mkono wanamgambo. Rwanda imekanusha shutuma hizo na kuishutumu DRC kwa kuunga mkono FDLR.


342/