Main Title

source : Parstoday
Jumatano

21 Septemba 2022

17:05:07
1307038

Umoja wa Afrika: Hatutaki kuwa chanzo cha kutokea vita vingine baridi

Mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika ametangaza upinzani wake dhidi ya mashinikizo yanayotolewa dhidi ya viongozi wa bara la Afrika yenye lengo la kuwataka watangaze wapo upande gani katika mzozo na vita vya Ukraine.

Rais Macky Sall wa Senegal amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kama ninavyomnukuu: "Nimekuja hapa ili niseme kwamba, Afrika imewekewa mashinikizo ya kihistoria ya kutosha na hivi sasa bara hili halitaki kuwa chanzo cha vita vipya baridi.

Kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa: Tunataka kumalizwa hitilafu na kuhiitimishwa uhasama huko Ukraine kama ambavyo tunataka mgogoro huo upatiwe ufumbuzi kupitia mazungumzo na hivyo kuzuia kutokea maafa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, bara la Afrika limeazimia kushirikiana na washirika wake wote kwa ajili kukidhi mahitaji mbalimbali na kutatua changamoto zilizopo.

Aidha amezungumzia matukio ya ugaidi na kueleza bayana kwamba, tatizo la ugaidi halilihusu bara la Afrika pekee, bali hili ni tishio la dunia nzima hivyo basi kuna haja kupitia asasai za kimataifa kama Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kukachukuliwa hatua za maana na madhubuti kwa ajili ya kung'oa mizizi ya ugaidi ambao unahatarisha maisha ya walimwengu wote.

342/