Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

22 Septemba 2022

16:42:13
1307313

DR Congo, Uganda zaendeleza operesheni za pamoja za kijeshi mashariki mwa Congo

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda zimerefusha kwa miezi miwili operesheni za pamoja za kijeshi zilizoanzishwa dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) mashariki mwa nchi, jeshi la DRC lilisema Jumatano.

Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa mkutano wa pili wa mawaziri wa nchi hizo mbili uliofanyika katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa kwa ajili ya kutathmini hali ya mambo.

Operesheni hizo katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri zilianzishwa mwishoni mwa mwaka jana kufuatia shambulio la mara tatu la bomu la kujitoa mhanga katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, ambapo watu saba waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Mwezi Juni, Jumuiya ya Afrika Mashariki iliidhinisha kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi ili kulinda amani nchini DRC huku kukiwa na ukosefu wa usalama na kuenea ghasia.

Ripoti zinasema, baada ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi kutoka DRC na Uganda,"imependekezwa kurefusha operesheni hizo kwa muda wa miezi miwili ikisubiri kutumwa kwa jeshi la kikanda la Jumuiya ya Afrika na kujumuishwa jeshi la Uganda katika jeshi la kikanda."

Mnamo Septemba 8, makubaliano ya hadhi ya kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki yalitiwa saini mjini Kinshasa.

Kundi la ADF ambalo limetokea Uganda limekuwa likieendesha ugaidi mashariki mwa Congo kwa zaidi ya miongo miwili.

Operesheni za kijeshi zilizoanzishwa na vikosi vya Kongo na Uganda hazijafanikiwa kuboresha hali ya usalama.

Shambulizi la hivi punde lilitokea Jumanne wakati washukiwa wa ADF walipochoma malori matano kwenye barabara ya Komanda-Mambasa katika jimbo la Ituri, na kumuua dereva wa lori wa Somalia, kulingana na vyanzo vya habari.

Magari hayo yalikuwa yakielekea Kisangani, kutoka Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri.

Wakati huo huo akihutubu Jumanne kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix-Antoine Tshisekedi  ameituhumu Rwanda hadharani kwamba, imevamia ardhi ya nchi yake.

Tshisekedi ameeleza kwamba, licha ya nia njema ya serikali yake na mkono wa amani ulionyooshwa na raia wa DRC, lakini shukurani za baadhi ya majirani zimekuwa ni kuunga mkono makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aidha amekariri madai ya kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa nchi, madai ambayo Rwanda tayari imeyakanusha.

Kwa upande wake, Rais Paul Kagame wa Rwanda ameutaka Umoja wa Mataifa kutafuta suluhisho na ufumbuzi wa ukosefu wa amani na usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika hotuba yake kwa viongozi katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Kagame ameushutumu umoja huo kwa kutumia michezo ya lawama baada ya kushindwa kutafuta suluhu ya ukosefu wa usalama katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


342/