Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

22 Septemba 2022

16:43:24
1307315

Tanzania na Msumbiji zatiliana saini makubaliano ya ulinzi na usalama

Serikali za Tanzania na Msumbiji zimetiliana saini makubaliano ya eneo la usalama na ulinzi pamoja na eneo la utafutaji na uokoaji kwa nia ya kuendelea kulinda mipaka baina ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yametiwa saini katika Ikulu ya Msumbiji jijini Maputo wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini humo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, “Ushirikiano wa kudumisha amani na utulivu kwa sababu Tanzania na Msumbiji katika eneo hili wanashirikiana na ni muhimu kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi na usalama, na tulianza tangu miaka ya 1980 na kuhakikisha tunapambana dhidi ya magaidi na aina yoyote ya uharamia.

“Kama alivyosema Rais Filipe Nyusi kupitia mahusiano haya tumeweza kutiliana saini eneo la usalama na ulinzi na utafutaji na uokoaji ni hatua ya muhimu katika kusonga mbele,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema kuwa, ili kupambana na ugaidi lazima uwepo ushirikiano na ili kufanikisha ni lazima zifuatwe taratibu za kisheria kwa kuwepo kwa mikataba.

Rais Nyusi ameongeza kuwa, mikataba hiyo inagusa mambo mengi likiwemo suala la madawa ya kulevya, usafirishaji wa binadamu na mambo yanayoendana na haya, eneo la biashara ambapo kumekuwa na mdororo katika nchi ya Msumbiji ambayo imekuwa ikipitia katika wakati mgumu yakiwemo mabadiliko ya hali ya hewa.

342/