Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

24 Septemba 2022

15:44:05
1307818

Mahakama CAR yabatilisha amri za rais Touadera za uundaji jopo la katiba mpya

Mahakama ya juu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imebatilisha amri za rais Faustin Archange Touadera za kuunda kamati ya kuandika upya katiba, jambo ambalo lilizua hofu kuwa kiongozi huyo anataka kuwania urais kwa muhula mwingine wa tatu.

Amri hizo "ni kinyume na katiba na ni batili", imetangaza Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kubainisha kuwa sheria ya msingi inaweza tu kurekebishwa baada ya Seneti kuundwa.Mnamo Agosti 27, wapinzani na mashirika ya kiraia yalifanya maandamano katika mji mkuu Bangui kupinga mabadiliko ya katiba.Rais Touadera mwenye umri wa miaka 65 alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016, kisha akachaguliwa tena katika uchaguzi uliogubikwa na utata mwaka 2020, lakini katiba ya sasa haimruhusu kuwania muhula wa tatu.

Katika miezi ya karibuni, Mamlaka za Jamhuri ya Afrika ya Kati ziliandaa maandamano ya kuunga mkono mabadiliko ya katiba ambapo zaidi ya watu 1,000 walijitokeza katika maandamano yaliyofanyika Agosti 6.

Chini ya wiki moja baadaye, raisTouadara alisema kwamba "sauti zaidi na zaidi zinapazwa kudai marekebisho ya katiba".

Mnamo mwezi Machi, chama chake cha Vuguvugu la Muungano wa Mioyo (MCU) kilijaribu kufuta kikomo cha mihula miwili ya urais wakati wa kilichoitwa "majadiliano ya jamhuri" yaliyosusiwa na wapinzani wengi.

Hata hivyo chama hicho kilirudi nyuma kwenye wazo lake hilo kutokana na maandamano ya umma na ukosoaji wa jamii ya kimataifa.

Touadera alishinda kwa kupata asilimia 53.16 ya kura katika uchaguzi wa muhula wa pili uliofanyika mwaka 2020 na ambao uligubikwa na utata kutokana na hali ya ukosefu wa usalama iliyokuwa imetanda katika nchi hiyo ambayo imekuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda wa muongo mzima.

Chini ya theluthi moja ya wapigakura waliweza kushiriki kwenye zoezi la upigaji kura katika nchi hiyo yenye takriban watu milioni tano ambayo Umoja wa Mataifa unasema ni taifa la pili kwa maendeleo duni duniani.../


342/