Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

24 Septemba 2022

15:44:39
1307819

Rais wa Guinea ya Ikweta mwenye miaka 80 kugombea tena urais kwa muhula wa sita

Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, ambaye ametawala Guinea ya Ikweta kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 43, atawania muhula mpya katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi Novemba.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue, ambaye pia ni mtoto wa Obiang.

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Twitter, Mangue amesema: "kwa sababu ya haiba yake, uongozi wake na uzoefu wake wa kisiasa", chama tawala kimemchagua kwa kauli moja Obiang kuwa mgombeaji wake katika uchaguzi wa Novemba 20".

Ukiondoa wafame, Rais Obiang mwenye umri wa miaka 80, ndiye mkuu wa nchi aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi duniani.

Chama chake cha Demokrasia ya Guinea ya Ikweta (PDGE) kinashikilia viti 99 kati ya 100 katika bunge la chini linalomaliza muda wake na viti vyote 70 vya Seneti.

Lakini hadi sasa haikuwa wazi ni nani angetangazwa kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa urais.

Wakati fulani, Teodoro Nguema Obiang Mangue, mwana tajiri wa Obiang, aliyepewa jina la utani "Teodorin" na anayependa sana kusafiri kwa ajili ya starehe na burudani, alionekana kuwa ndiye aliyepangwa kugombea katika uchaguzi huo. Hata hivyo mwishowe hakuchaguliwa kuwa mgombea mwaka jana.

PDGE ilikuwa vuguvugu pekee halali la kisiasa nchini Guinea ya Ikweta hadi mwaka 1991, wakati mfumo wa siasa za vyama vingi uilipoanzishwa.

Mara zote alizogombea urais, Obiang mwenyewe hajawahi kuchaguliwa kwa chini ya asilimia 93 ya kura.../

342/