Main Title

source : Parstoday
Jumapili

25 Septemba 2022

18:28:46
1308074

Mali yaituhumu Ufaransa kwamba, imeisaliti baada ya kuondoa majeshi yake

Kanali Abdoulaye Maiga, Waziri Mkuu wa Muda wa Mali ameituhumu Ufaransa kwamba, imelitelekeza taifa hilo la magharibi mwa Afrika na kwamba, nchi yake imesalitiwa.

Kanali Maiga amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba, Mali imesalitiwa baada ya jeshi la Ufaransa kuondoka nchini humo mapema mwaka huu. 

Maiga ameilaani Ufaransa kwa kile alichokiita uamuzi wa upande mmoja wa kuvihamishia katika nchi jirani ya Niger vikosi vyake vilivyosalia na kueleza kwamba, Ufaransa inajihusisha na ukoloni mamboleo na udhalilishaji.

Mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa waliondoka nchini Mali katikati ya mwezi uliopita wa Agosti na kuashiria mwisho wa Operesheni ya Barkhane katika nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika.

Mvutano kati ya Ufaransa na Mali ulipamba moto katika miezi ya hivi karibu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2021 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati Kanali Assimi Goïta alipotwaa madaraka ya nchi.

Viongozi wa kijeshi walio madarakani nchini Mali mwezi Agosti 2020 waliamua kusitisha ushirikiano na  Ufaransa na sasa wanashirikiana na Russia katika vita dhidi ya magaidi.

Hivi karibuni Mali ililitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano wa dharura ili kusitisha kile inachokitaja kuwa ni "vitendo vya uchokozi" vinavyofanywa na Ufaransa kwa kukiuka mamlaka yake na kuunga mkono makundi ya magaidi wakufurishaji na ujasusi.


342/