Main Title

source : Parstoday
Jumapili

25 Septemba 2022

18:34:10
1308083

Wapinzani waandamana Angola kupinga matokeo ya uchaguzi; walalamikia wizi wa kura

Maelfu ya wananchi wa Angola wameandamana wakipinga kile walichosema kuwa uchaguzi uliokuwa na dosari wa mwezi uliopita ambao ulikirejesha madarakani chama tawala cha MPLA.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakiimba kwa pamoja, “Wananchi hawako pamoja na MPLA, tunataka waondoke!".

Waandamanaji hao walikwenda moja kwa moja katika uwanja wa Uhuru ambao kwa kawaida chama cha MPLA hufanya mikutano ya hadhara na hafla za ushindi.

Maandamano hayo yalikuwa ya amani, ingawa wachambuzi wa mambo wanahofia kuna hasira ya kutosha na vijana kukerwa sana na hali ya maisha na kusababisha mambo kuweza kubadilika mara moja na kuwa ghasia.

Wengi wao walikuwa miongoni mwa vijana na wasio na ajira ambao wanahisi wameangushwa na MPLA, ambayo baadhi ya wanachama wake wamekuwa mabilionea kutokana na utajiri wa mafuta wa Angola huku wananchi walio wengi wanaishi katika umaskini.

Mahakama ya Katiba ya Angola imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 24, yaliyompa ushindi mgombea wa chama tawala cha MPLA, Rais Joao Lourenco.

Kwa mujibu wa matokkeo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE), chama tawala kilipata asilimia 51.17 ya kura dhidi ya asilimia 43.95 ya mpinzani mkuu ambaye ni Costa Junior wa Chama cha Umoja wa Kitaifa wa Uhuru wa Jumla wa Angola (UNITA).

342/