Main Title

source : Parstoday
Jumapili

25 Septemba 2022

18:34:39
1308084

Umoja wa Mataifa: Sudan inajongewa na maafa hatari ya kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametahadharisha kuwa, nchi ya Sudan inajongewa na maafa ya kibinadamu.

Ripoti ya mashirika hayo inaeleza kuwa, Sudan inakabiliwa na maafa ya kibinadamu kwa sababu ya mavuno duni, kupanda kwa bei ya mafuta, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na ukosefu wa misaada ya kifedha.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, karibu theluthi moja ya Sudan yenye takriban watu milioni 45 inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha kuwa, idadi ya watu wenye njaa huenda ikaongezeka mpaka milioni 18 ifikapo mwisho wa mwezi huu kama wafadhili hawatajitokeza kutoa fedha ili kuwasaidia wale wanaotaabika kwa uhaba wa chakula.

Kwa upande wake, Mandeep O’Brien, mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Sudan anasema nchi hiyo inakabiliwa na tatizo la utapiamlo pamoja na baa la njaa. 

O’Brien ameziambia duru za habari kwamba, watoto milioni tatu walio na umri wa chini ya miaka mitano wana utapiamlo uliokithiri nchini Sudan.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa, muda wa kutoa misaada ya kuokoa maisha kwa watu milioni 10.9 walio katika mazingira hatarishi unakwenda kwa kasi.

Wanaelezea kuwa ni 36% tu ya dola bilioni 1.9 za Umoja wa Mataifa zinazohitajika kuwasaidia wananchi hao ndiyo imetolewa hadi sasa.

342/