Main Title

source : Parstoday
Jumanne

27 Septemba 2022

18:14:52
1308674

UN yataka juhudi zaidi zifanyike ili kukomesha migogoro ya Sudan Kusini

Wataalamu wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu walionya kwamba mchakato wa amani wa Sudan Kusini unahitaji kuangaliwa haraka ili kuzuia ghasia kuzidi.

Yasmin Sooka, Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini, ametoa mwito huo kwa jamii ya ya kimataifa na kuutaka kuzingatia haraka zaidi ghasia zinazozidi kuongezeka katika kona mbalimbali za Sudan Kusini.

Sooka amesema wafadhili wakuu wa Sudan Kusini wanaendelea kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya amani na mageuzi katika sekta ya usalama ili kuhakikisha sheria ya kikatiba inapitishwa kabla ya uchaguzi.

Sooka amesema katika taarifa yake huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini kwamba, iwapo mwito anaotoa utapuuza na hakutachukuliwa hatua zozote, basi kuna uwezekano wa kuona mamilioni zaidi ya Wasudan Kusini wakikimbia makazi yao au kuvuka mipaka na kusababisha maafa kwa nchi jirani na kwa mashirika ya misaada. 

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa pia wamesema, pande zinazohusika katika Makubaliano ya wa Amani Yaliyofufuliwa mwaka 2018 nchini Sudan Kusini zilitia saini makubaliano ya kuongezwa muda wa miaka miwili utawala wa mpito na kuakhirishwa uchaguzi hadi mwishoni mwa 2024.

Makubaliano ya Amani yalijumuisha mchakato wa mashauriano wa kitaifa kuhusu kuanzisha Tume ya Ukweli, Mapatano na Ujenzi Mpya. Mashauriano yalifanyika katikati ya mwaka wa 2022 lakini yaliwatenga mamilioni ya wakimbizi ambao walikuwa wamekimbia maeneo yao wakihofia maisha yao na wakazi wa sehemu kubwa ya nchi wakiwemo wale wa maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa wapinzani.

342/