Main Title

source : Parstoday
Jumanne

27 Septemba 2022

18:19:35
1308683

UN: Ukame unaweka watoto milioni 3.6 katika hatari ya kuacha shule katika Pembe ya Afrika

Karibu watoto milioni nne wako katika hatari ya kuacha shule kutokana na ukame ulioliathiri eneo la Pembe ya Afrika. Hayo yamebainishwa katika taarifa ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa umesema kuwa suala hilo linaweza kupelekea kupotea kwa kizazi.

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linakadiria kuwa, watoto milioni 3.6 huko Kenya, Somalia na Ethiopia wako katika hatari ya kuacha shule katika misimi minne mtawalia ya ukame na hivyo kuzilemea familia. 

Mamilioni ya familia katika nchi hizo tatu za Pembe ya Afrika hivi sasa zimesukumwa katika ukingo wa umaskini na njaa. Abhiyan Jung Rana Mshauri wa Elimu wa shirika la UNICEF katika ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika amesema kuwa: katika eneo la Pembe ya Afrika kuna watoto wasiopungua milioni 15 ambao hawaendi shule. Wasiwasi uliopo ni kuwa, kutokana na ukame uliopo watoto wengine milioni 3.6 watashindwa kwenda shule kutokana na kuhamahama na wazazi wao wakielekea katika maeneo tofauti mbali na shule. 

Watoto wa kike ni wahanga wakuu wanaoathiriwa na ukame; ambapo walimu na wanaharakati huko Somaliland wanasema kuwa ni mabinti ndio wanaoacha shule kwa kiasi kikubwa kutokana na ukame. 

Shirika la UNICEF aidha limeongeza kuwa, ukosefu wa programu za kulisha chakula wanafunzi shuleni, na wazazi kutokuwa na uwezo wa kumudu mahitaji muhimu kama vile vitabu pia ni miongoni mwa mambo yanayoongeza uwezekano wa mtoto kuacha shule.

342/