Main Title

source : Parstoday
Jumatano

5 Oktoba 2022

15:42:08
1310805

Hamas yamkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza aliyesema yeye ni "Mzayuni mkubwa"

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imemkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss kwa kujiita "Mzayuni mkubwa" anayetaka kuimarisha uhusiano wa London na Tel Aviv, ikisema matamshi hayo yanalingana na Azimio la Balfour la Uingereza la 1917, ambalo liliweka msingi wa kuundwa utawala bandia wa Israel na kukoloniwa Palestina.

Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema katika taarifa yake kwamba "Matamshi  yaTruss kuhusu kuunga mkono Uzayuni yanamaanisha kuwa anasimama upande wa utawala wa Kizayuni na anaunga mkono uchokozi dhidi ya taifa la Palestina,"

Ameongeza kuwa matamshi hayo yanawiana na jinai za Uingereza zilizoanza zaidi ya miaka 100 iliyopita kwa Azimio la Balfour ambalo ni dhidi ya taifa la Palestina ambalo sasa linapinga kuvamiwa na kukoloniwa ardhi zake na utawala haramu wa Israel.

Afisa huyo wa Hamas amesema Waziri Mkuu wa Uingereza ni mmoja wa wale wanaoficha mauaji ya watoto wasio na hatia, na kuongeza kuwa tamko la Truss, "ni aibu kwa ubinadamu."

Azimio la Balfour lilikuja kwa njia ya barua kutoka kwa waziri wa mambo ya nje wa Uingereza wakati huo, Arthur Balfour, iliyoelekezwa kwa Lionel Walter Rothschild, mkuu wa jumuiya ya Mayahudi wa Uingereza. Barua hiyo ilichapishwa mnamo Novemba 2, 1917.

Tamko hilo lilitolewa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dudunia (1914-1918) na lilijumuisha maelezo kuhusu Uingereza kuitawala Palestina baada ya kuvunjika kwa Dola la Otthmaniya.

Azimio la Balfour linatajwa kuwa utangulizi wa tukio la Nakba huko Palestina mwaka 1948, wakati vikundi vya kijeshi vya Kizayuni vilivyojizatiti kwa silaha, vilivyopewa mafunzo na kuundwa kupigana bega kwa bega na Waingereza katika Vita vya Pili vya Dunia, vilipowafukuza kwa nguvu zaidi ya Wapalestina 750,000 kutoka nchi yao.

Akizungumza katika hafla ya Marafiki wa Kihafidhina wa Israel (CFI) wakati wa mkutano wa Chama cha Conservative huko Birmingham, Truss ameonyesha uungaji mkono wake usioyumba kwa Israel.

"Nimefurahi sana kuwa hapa kwa mara ya kwanza katika hafla ya CFI kama waziri mkuu wako," alisema Jumapili.

"Kama unavyojua mimi ni Mzayuni mkubwa, mimi ni mfuasi mkubwa wa Israeli, na ninajua kwamba tunaweza kuchukua uhusiano wa Uingereza na Israeli kutoka nguvu hadi nguvu."

Mwezi uliopita, Truss alimwambia waziri mkuu wa Israel Yair Lapid kwamba anafikiria kuhamisha ubalozi wa Uingereza mjini Tel Aviv hadi mji mtakatifu wa al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel. Iwapo hilo litafanyika, mabadiliko ya sera yenye utata yatakuwa sawa na yale ya Marekani chini ya aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump mwezi Mei 2018. Wapalestina wameungana katika kulaani pendekezo hilo la waziri mkuu wa Uingereza.