Main Title

source : Parstoday
Jumatano

5 Oktoba 2022

15:43:25
1310808

Russia: Msaada wa silaha wa Marekani kwa Ukraine unaiweka Russia na NATO katika makabiliano ya kijeshi

Afisa wa ngazi za juu wa serikali ya Russia amekosoa misaada ya silaha ya Marekani kwa Ukraine, akisema inaziweka Moscow na NATO kwenye ncha ya makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi.

Konstantin Vorontsov, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Kuzuia Uenezi na Udhibiti wa Silaha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, amesisitiza katika mkutano wa Tume ya Kwanza ya Umoja wa Mataifa kwamba misaada ya silaha ya Marekani kwa Ukraine itasababisha mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi kati ya Russia na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO).

Matamshi hayo yametolewa siku chache baada ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova kusema kuwa: Marekani haina kikomo katika hutumia mbinu yoyote kwa ajili ya kuisukuma Russia kwenye matumizi ya silaha za nyuklia.

Zakharova aliongeza kuwa, Washington imetumia mbinu zake zote bila kikomo kuilazimisha Moscow kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

Rais wa zamani wa Russia, Dmitry Medvedev hivi karibuni alizionya nchi za Ulaya na Marekani akisema kuwa, kwa mujibu wa stratijia za kiulinzi za Russia, Moscow ina haki ya kujihami kwa silaha zozote zile zikiwemo za atomiki iwapo itakuwa chini ya shinikizo kubwa.

Ikumbukwe kuwa uamuzi wa mwisho wa kutumia silaha za nyuklia kwa mujibu wa katiba ya Russia umo mikononi mwa rais wa nchi hiyo ambaye hivi sasa ni Rais Vladimir Putin.

342/