Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:30:59
1311130

Kung'ang'ania Biden kuiwekea vikwazo vipya Tehran, dhihirisho la uadui kwa wananchi wa Iran

Rais wa Marekani, Joe Biden, siku ya Jumatatu ya tarehe 3 Oktoba 2022, alijitokeza hadharani bila ya haya na kuunga mkono machafuko na kuuliwa maafisa usalama na wananchi wa Iran katika vurugu za hivi karibuni.

Biden hakuishia hapo bali alisema kuwa, Marekani imeamua kuiwekea Iran vikwazo vipya akidai kuwa inaweka vikwazo hivyo eti kuwalinda wananchi wa Iran. Pia alisema Marekani itawarahisishia Wairan mitandao ya kijamii inayochochea machafuko humu nchini. 

Kabla ya hapo, wizara ya hazina ya Marekani ilitangaza kukiwekea vikwazo kikosi cha usalama wa kimaadili cha jeshi la polisi la Iran kwa kutoruhusu wanawake watembee uchi humu nchini. Pia Marekani ilidai kuwa kikosi hicho cha jeshi la polisi la Iran kimehusika na kifo cha Mahsa Amini bila ya kutoa chembe ya ushahidi.

Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran na vitisho vipya vya Biden kwa hakika si jambo geni hata kidogo. Kwa zaidi ya miaka 40, Iran iko chini ya vikwazo vya kiholela na vya upande mmoja vya Marekani. Vikwazo vya Marekani wakati wa utawala wa Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilitia fora kuliko wakati mwingine wowote. Washington iliwawekea wananchi wa Iran vikwazo vikali mno na kujigamba kuwa haitoruhusu hata tone moja la mafuta ya Iran liuzwe nje ya nchi. Leo viongozi hao hao wa Marekani wanajitokeza hadharani na kudai bila haya kuwa eti wanawapenda wananchi wa Iran. Vikwazo hivyo vikali mno vya Marekani viliwekwa dhidi ya Iran baada ya kuondolewa kwake kufuatia mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Marekani yenyewe ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha. Rais wa hivi sasa wa Marekani anaendeleza vikwazo hivyo licha ya kukiri kwamba wameshindwa kulizuia taifa la Iran kujitegemea na kujiletea maendeleo. Mara baada ya kuingia madarakani, Biden alidai kuwa, serikali yake ni tofauti na serikali ya Donald Trump, lakini hivi sasa si tu haijaondoa vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa na Trump, bali ndio kwanza inaendelea kuiwekea Iran vikwazo vipya kwa visingizio chapwa. Mara hii Marekani imetumia kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini na inawaunga mkono waziwazi magaidi na wafanya fujo nchini Iran.

Labda msikilizaji mpenzi, utajiuliza ni nini hasa lengo la siasa hizi za kibeberu za Marekani dhidi ya taifa la Iran? Lengo la Washington liko wazi. Lengo lake ni kutaka kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndio maana upande mmoja inatangaza kuiondolea vikwazo vya Intaneti Iran ili maadui wapate nguvu za kuchochea machafuko kupitia mawasiliano ya Intaneti na wakati huo huo lakini inaweka vikwazo vipya dhidi ya wananchi wa Iran ambayo ndivyo hasa vinavyopaswa kuondolewa kama kweli Marekani ina nia njema. Hivi sasa Marekani imeona vikwazo vyake dhidi ya Iran vimepungua makali hivyo imeamua kuendeleza vikwazo vya Donald Trump kwa madai ya kuunga mkono wananchi wa Iran.

Kit Klarenberg mwandishi wa habari wa Uingereza anasema: Siri ya vita vya Intaneti vya Pentagon (Wizara ya Ulinzi ya Marekani) dhidi ya Iran ni kugonga kwenye kitufe kimoja tu ukiwa Marekani na kusubiri uone machafuko yanavyotokea Tehran. Machafuko mapya nchini Iran yamepangwa na kuchochewa na madola ya kigeni.

Ukweli ni kuwa, madai ya rais wa Marekani ya kujifanya kuwa anawapenda wananchi wa Iran ni uongo ulio wazi kabisa. Wananchi wa Iran hawawezi kabisa kusahau jinai na ubeberu wa Marekani dhidi yao wa kipindi cha miaka 80 sasa. Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu Iran wakati Washington iliposhirikiana na Waitifaki katika Vita vya Pili vya Dunia. Uvamizi huo wa Marekani uliwasababishia misiba na matatizo mengi wananchi wa Iran. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia pia, yaani mwaka 1953, Marekani ilishirikiana na Uingereza  kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran na kumpindua Waziri Mkuu wa wakati huo, Dk Mohammad Mosadiq kwa madhara ya wananchi wa Iran. Kwa hakika jinai za Marekani dhidi ya wananchi wa Iran ni nyingi na ni kubwa sana, hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na hatuwezi kumaliza kuzitaja. Kiujumla ni kwamba, kujitokeza kiongozi wa Marekani na kudai kuwa anawapenda wananchi wa Iran, kwa kweli ni kichekesho kikubwa, bali ni kebehi kwa wananchi wa taifa hili kubwa la Kiislamu.


342/