Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:31:27
1311131

Pyongyang yavurumisha tena makombora ya balestiki kujibu chokochoko za US

Kwa mara nyingine tena, Korea Kaskazini imefyatua makombora yake ya balestiki kuelekea upande wa Japan, kujibu chokochoko mpya za Marekani dhidi ya Pyongyang.

Mkuu wa Majeshi ya Japan amesema, makombora hayo ya masafa mafupi yamevurumishwa mapema leo Alkhamisi kuelekea upande wa Japan, yakitokea pwani ya mashariki ya Korea Kaskazini.

Serikali ya Pyongyang imechukua hatua hiyo baada ya manowari ya Marekani ya USS Ronald Reagan yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita kuelekezwa katika maji ya Peninsula ya Korea.

Aidha Korea Kaskazini imevurumisha makombora hayo ya balestiki siku chache baada ya Korea Kusini, Japan na Marekani kufanya luteka ya kijeshi ya 'kupambana na nyambizi' katika Peninsula ya Korea.

Hii ni mara ya sita kwa Korea Kaskazini kufyatua makombora ya balestiki ndani ya siku 12. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, Korea Kaskazini imefanya majaribio zaidi ya 20 ya silaha zake huku sehemu kubwa ya majaribio hayo ikiwa ni kufyatua makombora ya balestiki.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amelaani kitendo hicho na kusema kuwa, "Hii ni mara ya sita ndani ya siku chache tokea mwishoni mwa Septemba, kwa Korea Kaskazini kuchukua hatua kama hii. Hili ni jambo lisilokubalika."

Juzi Jumanne,  Pyongyang ilivurumisha kombora lake la balestiki la masafa ya kati (IRBM), lililopaa katika anga ya maeneo ya kaskazini mwa Japan. Wiki iliyopita pia, Korea Kaskazini ilifyatua makombora mengine ya balestiki, saa chache baada ya Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani kuondoka Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini.

342/