Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:31:56
1311132

Utafiti: Mitazamo hasi dhidi ya Waislamu inaenea kwa kasi Ujerumani

Mitazamo hasi na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka kwa kiwango cha kutia wasiwasi nchini Ujerumani.

Utafiti mpya uliofanywa na Baraza la Wataalamu la Utangamano na Uhamiaji la Ujerumani (SVR) umeonesha kuwa, asilmia 48 ya Wajerumani wanahisi kuwa Uislamu 'hauendani' na jamii ya Ujerumani.

Aidha asilimia 29 ya Wajerumani walioshirikishwa kwenye utafiti huo wanasisitiza kuwa dini ya Kiislamu inapaswa kupigwa marufuku nchini humo.

Utafiti huo umebainisha kuwa, mitazamo hiyo ya chuki za kidini inawalenga Waislamu wa matabaka yote, wawe wahajiri au wazawa wa nchi hiyo ya Ulaya.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa taasisi ya Expert Council on Integration and Migration (SVR), asilimia 44 ya washiriki wanataka mashirika na jumuiya za Kiislamu zifuatiliwe na serikali.

Mwezi Juni mwaka huu, shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini Ujerumani liliripoti kuwa limesajili matukio zaidi ya 800 ya kushambuliwa misikiti na maeneo matakatifu ya Waislamu nchini humo.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, Ujerumani yenye jamii ya watu milioni 84, ndilo taifa la pili lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu Ulaya Magharibi baada ya Ufaransa. Nchi hiyo ina Waislamu karibu milioni 5, na idadi hiyo inaongezeka kwa kasi kubwa. 


342/