Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:32:19
1311133

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Dunia haijasahau kashfa ya makaburi ya halaiki nchini Canada

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema: Ulimwengu bado haujasahau kashfa ya kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki ya mamia ya watoto katika viwanja vya shule za wamishonari yapata mwaka mmoja uliopita.

Nasser Kan'ani Chafi ameandika katika ukurasa wake wa Instagram siku ya Alkhamisi kufuatia uingiliaji wa serikali ya Canada katika masuala ya ndani ya Iran kwamba: "Wakati haki za binadamu zinapokuwa wenzo na chombo cha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya nchi nyingine, vyombo vya habari vya mfumo wa ubeberu pia husaidia kuwafanya wale wanaotuhumiwa kwa ukiukaji wa kimfumo wa haki za binadamu waonekane kama watetezi wa haki hizo."

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ambaye alikuwa akijibu hatua ya serikali ya Canada ya kuziweka vikwazo taasisi na watu mbalimbali wa Iran kutokana na madai ya "ukiukaji wa haki za binadamu" ameongeza kuwa: "Dunia bado haijasahau historia ya kutenganishwa kwa lazima watoto zaidi ya 150,000 wa wakazi asili wa Canada na familia zao na kugunduliwa kwa makaburi ya umati yenye mabaki ya mamia ya watoto hao kwenye viwanja vya shule za wamishonari huko Canada takriban mwaka mmoja iliyopita."

Kanani Chafi amesema: "Kueneza maneno ya uongo kuhusu nchi nyingine hakubadili ukweli kwamba, makavazi ya haki za binadamu ya mmoja wa washirika wa karibu wa serikali ya Marekani, yanadhihirisha mauaji ya watoto wachanga na kukanyagwa kwa ubinadamu."

Kugunduliwa makaburi ya halaiki na miili ya mamia ya watoto nchini Canada kumeibua kashfa ya mauaji na ubaguzi mkubwa wa rangi uliofanywa na Kanisa Katoliki likishirikiana na serikali ya Canada dhidi ya wenyeji asili wa nchi hiyo.

Ukubwa wa janga hilo uliwapelekea wanaharakati wa mashirika ya kiraia ya Canada na viongozi wa kisiasa nje ya mipaka ya Canada kulalamikia vikali jinai hiyo kiasi kwamba Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, alilazimika kukosoa uzembe uliofanywa na serikali ya Canada na pia kulibebesha Kanisa Katoliki dhima ya maangamizi hayo ya umati.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Canada, Jumatatu iliyopita alitangaza kifurushi kipya cha vikwazo dhidi ya Iran  kwa kutumia kisingizio cha kifo cha "Mehsa Amini" aliyeaga dunia akiwa kwenye kituo cha polisi wa maadili.

342/