Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:33:10
1311135

Abdollahian: Serikali itakabiliana na wafanya fujo, magaidi kwa misingi ya sheria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameuonya Umoja wa Ulaya dhidi ya kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, serikali ya Tehran itakabiliana na wafanya fujo na magaidi kwa kuzingatia misingi ya sheria za nchi hii.

Hossein Amir-Abdollahian alitoa indhari hiyo jana Jumatano katika mazungumzo yake ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa, Iran itatoa jibu mwafaka iwapo EU itachukua uamuzi wa kisiasa ulioharakishwa, mkabala wa ghasia zinazoshuhudiwa hapa nchini.

Kauli ya Abdollahian imetolewa siku moja baada ya mwanadiplomasia huyo Umoja wa Ulaya kusema kuwa, EU inatafakari suala la kuiwekea Iran vikwazo, eti kutokana na kifo cha binti Muirani Mahsa Amini, na eti kwa kukandamizwa maandamano ya kulaani kifo hicho.

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, Idara ya Mahakama ya Iran inachunguza kifo hicho kwa mujibu wa sheria za nchi hii, na matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, wananchi wa Iran wana haki ya kudai wanachotaka kwa amani, na daima serikali imekuwa ikiwasikiliza.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, kufanya maandamano ya amani hakufungamani kabisa na wafanya fujo kuchoma moto ambulensi, kushambulia benki na maeneo ya umma, kushambulia maafisa usalama na raia wengine, na kufanya vitendo vya kigaidi.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameunya Umoja wa Ulaya dhidi ya kuchukua hatua ya kisiasa kwa pupa, kwa kutegemea madai yasiyo na msingi, yenye shabaha ya kuwachochea wafanya ghasia na magaidi ili waendelee kuhatarisha usalama na maisha ya Wairani.

Kwa upande wake, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema anakubaliana na ukweli kwamba, ugaidi ni tofauti na maandamano ya amani. Amesema EU haina nia ya kuibua matatizo katika uhusiano wake na Iran.

Wawili hao wamejadili pia kadhia ya kuondolewa Iran vikwazo vya kidhalimu, na wamesema wanaridhishwa na hatua zilizopigwa kwenye mazungumzo hayo.

342/