Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

6 Oktoba 2022

18:35:32
1311138

Sababu na matokeo ya kushindwa kwa usitishaji vita nchini Yemen

Mazungumzo ya kurefusha usitishaji vita kwa mara ya tatu nchini Yemen yameshindwa kufikia mwafaka.

Makubaliano ya kusitishaji vita nchini Yemen yalifikiwa mwishoni mwa mwaka wa saba wa vita vya muungano wa Saudia dhidi ya nchi hiyo kwa upatanishi wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, na yalianza kutekelezwa tarehe 2 Aprili kwa miezi miwili na kurefushwa mara nyingine. Usitishaji huo wa mapigano ulitekelezwa katika hali ambayo, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Yemen ilikuwa ikikabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu kuwahi kutokea duniani kutokana na vita vilivyoendelea kwa miaka 7. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kwa nini usitishaji huo wa mapigano haujarefushwa tena au haujafanywa usitishaji wa kudumu wa mapigano?

Sababu ya kwanza ni kwamba, lengo la kusimamisha vita lilikuwa kusitisha mapigano kwanza na kisha kutayarisha mazingira ya kutumwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Yemen. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi 6 iliyopita, Wayemeni wametahadharisha mara kwa mara kuhusu ukiukwaji wa usitishaji vita unaofanywa na Saudi Arabia na kutangaza kuwa, Riyadh na washirika wake hawazingatii masharti ya usitishaji vita. Ingawa usitishaji vita huo umesababisha ahueni katika vita vya Yemen, lakini Saudia imekataa kuondoa mzingiro wa Bandari ya Al Hudaydah na kuruhusu kutumwa kwa misaada ya kibinadamu kwa njia ya upendeleo wa maeneo maalumu,;suala ambayo halikuwa na athari kubwa katika kupunguza mzozo na matatizo watu wa Yemen. 

Aidha usitishaji huo wa mapigano haukuwawezesha Wayemeni kuuza mafuta yao wao wenyewe na kuweza kulipa mishahara ya wafanyakazi na kukidhi baadhi ya mahitaji yao. Kwa hakika usitishaji vita na kusimamishwa mashambulizi ya kulipiza kizazi ya Yemen kumeipa Saudia na Imarati fursa nzuri ya kupora rasilimali za mafuta za Yemen kwa urahisi zaidi na kuwanyima Wayemeni mapato yao ya mafuta. Saudia inaona kuwa, kuiruhusu Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen kutumia mapato ya mafuta kunaweza kuipa kibali na uhalali zaidi, na jambo hilo linakinzana na maslahi ya Riyadh na washirika wake. 

Sababu nyingine ya kufeli usitishaji vita huko Yemen ni kwamba, kwa mtazamo wa Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen, Saudi Arabia imetumia usitishaji vita kama fursa ya kujiimarisha kijeshi na kuzuia mashambulizi ya Wayemeni.

Kwa kuzingatia sababu hizo, Hisham Sharaf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen, anasema kuwa upande wa Saudia hauna nia ya kweli ya kutafuta suluhu la mgogoro wa Yemen.

Mwishoni inatupasa kusema kuwa, kufeli kwa usitishaji vita nchini Yemen kunaweza kuzidisha matatizo na mgogoro wa binadamu katika nchi hiyo na kusababisha duru mpya ya mashambulizi ya Wayemeni dhidi ya Saudia na Imarati.

Kuhusiana na hilo, Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen amezionya kampuni zote za mafuta huko Imarati na Saudi Arabia na kuzitakka ziondoke katika nchi hizo haraka iwezekanavyo.

342/