Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

8 Oktoba 2022

20:54:32
1311723

UN: Watu karibu milioni 4 wanabikiliwa na utumwa mamboleo Afrika

Taasisi za Umoja wa Mataifa zimetoa ripoti mpya inayoonesha kushamiri kwa utumwa mamboleo katika nchi za Afrika, ambapo katika kila watu 1000, 29 wanafanyishwa kazi za sulubu barani humo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), Shirika la Wahajiri Duniani (IMO) na taasisi ya Walk Free umefichua kuwa, watu milioni 3.8 walikuwa wakiishi katika utumwa mamboleo hadi kufikia mwaka jana 2021 barani Afrika.

Ripoti hiyo inasema, ndoa na kazi za kulazimishwa ziliongezeka sana mwaka jana kutokana na sababu kadhaa, hususan janga la Corona na athari zake kwa uchumi na soko la ajira barani Afrika na kote duniani.

Imesema mwaka jana kulishuhudiwa ongezeko la watoto kulazimishwa kuingilia biashara haramu ukahaba katika maeneo yanayoshuhudia vita na migogoro kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Sudan, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Licha ya ongezeko hilo, lakini Afrika linasalia kuwa bara linalosajili viwango vya chini vya utumwa duniani, yaani asilimia 2.9 kwa kila watu 1000. Nchi za Kiarabu zinaongoza kwa asilimia 5.3 katika kila watu 1000, Ulaya na Asia ya Kati asilimia  4.4, huku Amerika ya Kusini na Kaskazini, Asia na Pacific zikisajili asilimia 3.5.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa anuani isemayo "Makadirio ya Utumwa Mamboleo Duniani 2021; Kazi na Ndoa za Lazima, watu milioni 50 walikuwa wakiishi katika utumwa mamboleo hadi kufikia mwaka jana 2021 kote duniani, ambapo milioni 28 walikuwa katika kazi ya kulazimishwa na milioni 22 wakiwa katika ndoa za lazima.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, wafanyakazi wahamiaji wana uwezekano mkubwa zaidi ya mara tatu kuwa katika kazi za kulazimishwa kuliko wafanyakazi wasio wahajiri.

342/