Main Title

source : Parstoday
Jumapili

9 Oktoba 2022

19:57:16
1312052

Tangazo la Rais wa Tunisia la marekebisho ya sheria ya uchaguzi

Ofisi ya Rais wa Tunisia imetangaza katika taarifa yake kwamba Rais Kais Saied, ameamua kurekebisha sheria ya uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo.

Taarifa hiyo imemnukuu Kais Saied akisema: Marekebisho haya yanafanywa ili kuzuia uhalifu na pia kukomesha uenezaji wa "fedha za kifisadi". Kais Saied ameendelea kwa kusema: Kukomesha suala hili ni "wajibu wa kitaifa".

Harakati ya Ennahda imejibu uamuzi huo wa Kais Saied kwa kuonya kuhusu hatari ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi. Harakati hiyo pia imetoa wito wa kuunganisha pamoja juhudi za kukabiliana na "mapinduzi" na kuzidisha maandamano ya amani dhidi ya mfumo unaotawala nchini humo.

Kais Saied alichukua udhibiti wa nchi hiyo ndogo ya Afrika Kaskazini mnamo Julai 25, 2021 katika hatua iliyotambuliwa na vyama vya siasa kuwa ni mapinduzi dhidi ya serikali na katiba ya nchi. Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Saied alilitimua Bunge na kumfuta kazi Spika na Waziri Mkuu na baadaye akadhibiti mambo yote ya nchi hiyo. Kisingizio kilichotumiwa na Kais Saied ni kwamba waziri mkuu na serikali ya nchi hiyo imeshindwa kuboresha hali ya uchumi na kukabiliana vilivyo na janga la virusi vya corona. Hatua hii imesababisha mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Tunisia na inaweza kutambuliwa kuwa mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa nchini humo tangu baada ya vuguvugu la wananchi mwaka 2011. Mwezi Julai mwaka huu pia aliitisha kura ya maoni ya katiba mpya ambayo ilisusiwa na akthari ya Watunisia. Hamadi El-Disi, profesa wa sayansi ya siasa nchini Tunisia, anasema: "Tofauti na kura ya maoni ya katiba mwaka 2014, mara hii hapakuwa na mjadala mkali na wa umma kuhusu rasimu iliyopendekezwa kwa ajili ya katiba mpya ya Tunisia".

Licha ya kuanza kutekelezwa kwa katiba mpya, maandamano dhidi ya Rais Qais Saied yanaendelea. Wapinzani wanaitambua hatua yake kuwa ni  dhidi ya malengo ya mwamko wa wananchi mwaka  2011 na juhudi za kuanzisha demokrasia nchini Tunisia.

Meytham Qassemi, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tunis, anasema kuhusiana na hili kwamba: "Demokrasia ya Tunisia kwa mara nyingine tena iko katika njia panda na hatari. Hatua ya Rais wa Tunisia kuidhinisha katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyokumbwa na utata mkubwa inaonyesha kuwa nchi  kwa mara nyingine iko katika njia ya udikteta baada ya miaka kumi ya demokrasia ya kweli."

Chama cha Ennahda, kikiwa ni chama kikubwa na chenye ushawishi mkubwa nchini Tunisia, kilitangaza katika taarifa yake mpya kwamba katiba mpya si suluhisho la matatizo ya nchi, bali inaimarisha dhulma, ukandamizaji na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. 

Kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya Tunisia ilifanyika Julai 25 huku kukiwa na hali ya kutoridhika, na maandamano ya wananchi na viongozi wa vyama vingi vya upinzani. Kura hiyo ya maoni ilisusiwa na makundi makubwa ya kisiasa na vyama vya nchi hiyo kama vile Ennahda, Moyo wa Tunisia, Muungano wa Heshima, Harakati ya Irada na Matumaini ya Tunisia, Chama cha Republican, Harakati ya Demokrasia, Harakati ya Demokrasia ya Kazi na Uhuru, na Chama cha Leba. Vyama hivyo vya upinzani vinasisitiza kuwa mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba ulikiuka sheria.

Kulingana na ripoti ya Baraza la Uchaguzi la Tunisia, kiwango cha ushiriki katika kura ya maoni ya katiba mpya ya Tunisia kilitangazwa kuwa karibu 27%, ambayo ilikuwa uthibitisho wa kutoshiriki katika zoezi hilo ambalo liliitishwa na rais wa Tunisia.

Kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge ni hatua nyingine "isiyo ya kawaida" ya Rais wa Tunisia, ambayo kulingana na uamuzi wake itafanyika tarehe 17 Disemba.

Sasa inaonekana kuwa lengo la Kais Saied kutangaza marekebisho ya sheria ya uchaguzi, ni kuwafutilia mbali wapinzani wake wote muhimu wa kisiasa; na kwa kuzingatia nafasi kubwa na muhimu ya chama cha Ennahda katika uwanja wa siasa wa Tunisia, kiongozi huyo anajaribu kwa kila njia kuwazuia wagombea wa chama hicho wasiingie kwenye uwanja wa uchaguzi. Hapo awali, Rais wa Tunisia alizindua jitihada za wazi za kuiondoa Ennahda katika uga wa siasa wa Tunisia kwa kufuta jina la Uislamu kwenye katiba ya nchi hiyo. Vilevile ametumia vibaya mahakama ya nchi kwa ajili ya kumkamata na kumhukkumu mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Ennahda, Rached Ghannouchi. Hata hivyo, hatua hizi zimekabiliwa na upinzani mkubwa, na majaji wa Tunisia wamekosoa mara kwa mara uingiliaji kati wa Rais katika utendaji wa taasisi hiyo na mashinikizo yake dhidi ya majaji. 

Mapema mwezi Juni, Kais Saied aliwafukuza kazi majaji 57 kwa tuhuma za rushwa na kuzuia uchunguzi wa mahakama. Mikakati hiyo ya kudhoofisha taasisi ya Mahakama ya Tunisia, pamoja na kusimamishwa shughuli za Bunge imefunga njia ya kujitokeza upinzani wowote wa kisheria dhidi ya utawala wa Kais Saied nchini Tunisia.

Kwa ujumla, inatupaswa kusema kwamba, hatua za Kais Saied katika kipindi cha mwaka na miezi kadhaa iliyopita zimelenga kujilimbikizia madaraka mikononi mwake na kuwafuta wapinzani wake wa kisiasa.