Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

10 Oktoba 2022

18:55:05
1312391

Kenya na Tanzania zaazimia kuimarisha uhusiano katika safari ya Ruto

Rais William Ruto wa Kenya leo ametembelea Tanzania na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Baada ya mazungumzo hayo, wawili hao wamehutubua waandishi habari Ikulu mjini Dar es Salaam na kubainisha nukta kadhaa muhimu.   Marais hao wametoa maagizo kwa mawaziri wa uwekezaji kuhakikisha wanaondoa vikwazo 14 vya biashara baina ya nchi hizo.

Rais wa Kenya amesema yale mabishano yaliyokuwepo baina ya Tanzania na Kenya wameyaweka nyuma.

Rais Ruto aidha amebaini kuwa wanataka kujenga uchumi wa pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na yapo mengi watayafanya wakiwa pamoja.

Huku akimhakikishia Rais Samia kuwa binafsi atashirikiana kufanikisha waliyokubalian ameongeza kuwa serikali yake ipo tayari kufanya kazi kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Ruto ameongeza kuwa biashara baina ya Tanzania na Kenya imezidi kuimarika ambapo usafirishaji wa bidhaa kwa mwaka mmoja imepanda kutoka Sh27 bilioni kutoka Tanzania kufikia Sh50 bilioni kwenda Kenya.

Rais Samia amesema ziara ya Ruto inatoa fursa ya kutathimini fursa ya ushirikiano katika ngazi zote. “Tanzania na Kenya tusigawane umasikini na udhalili lakini tugawane utajiri tutakaofanya kupitia biashara,” amesema Rais Samia.

Aidha Rais Samia “Mawaziri walitambua vikwazo 68 na vilifanyiwa kazi 54 na tumewataka sasa mawaziri wetu wakutane na kufanyia kazi vikwazo hivyo ili kuwe na uhuru wa kibiashara."

Rais Ruto ameitembelea Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo aliwasili jana na leo amekutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kufanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam.

342/