Main Title

source : PARSTODAY
Jumanne

11 Oktoba 2022

17:05:37
1312712

Mazungumzo muhimu ya maridhiano ya kitaifa ya Wapalestina kuanza leo nchini Algeria

Wajumbe wanaoziwakilisha harakati za muqawama za Palestina za Hamas na Jihadul-Islami wamewasili Algiers mji mkuu wa Algeria kwa lengo la kushiriki mazungumzo muhimu ya maridhiano ya kitaifa ya Wapalestina.

Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul-islami Anwar Abu Taha alitangaza usiku wa kuamkia leo kuwa ujumbe wa harakati hiyo umeelekea Algeria kwa mwaliko wa Rais Abdelmadjid Tebboun wa nchi hiyo na kwa lengo la kushiriki mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa ya Palestina.

Abu Taha amebainisha kuwa, Jihadul-Islami kila mara imekuwa ikikaribisha na kuunga mkono juhudi zozote zinazofanywa kwa lengo la kuondoa tofauti za ndani na kuleta mapatano na maridhiano ya kitaifa ya Palestina.

Wakati huohuo, Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS naye pia amewasili nchini Algeria akiongozana na maafisa wa ngazi za juu wa harakati hiyo. Hamas imetangaza kuwa, Haniya na ujumbe aliofuatana nao wameelekea Algeria kushiriki mazungumzo ya mapatano ya kitaifa ya Palestina.

Fayez Abu Ai'tah, balozi wa Palestina nchini Algeria amesema, mazungumzo ya makundi ya Palestina yanaanza leo na yataendelea hadi kesho katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Abu Ait'ah amebainisha kuwa, wawakilishi wa makundi 12 ya ukombozi wa Palestina wakiongozwa na harakati za Fat-h, Hamas na Jihadul-Islami watahudhuria vikao vya mkutano huo ambao unafanyika baada ya jitihada za miezi kadhaa zilizofanywa na Algeria kwa madhumuni ya kutafuta muelekeo jumuishi wa mustakabali na makubaliano yatakayoridhiwa na pande zote za kitaifa za Palestina.

Awali kabla ya hapo, Rais Abdelmadjid Tebboun wa Algeria alitoa kauli akisisitiza kuwa nchi yake haitaruhusu Palestina ikoloniwe.

Kwa mujibu wa viongozi wa Algeria mkutano wa makundi ya Palestina ni utangulizi wa mkutano wa wakuu wa nchi za Kiarabu ambao serikali ya Tebboun imeupa jina la "mkutano wa kuiunga mkono Palestina".../

342/