Main Title

source : PARSTODAY
Jumanne

11 Oktoba 2022

17:06:33
1312715

Maiti 8 za wahajiri zapatikana pwani ya kusini ya Tunisia

Wavuvi wa Tunisia wameopoa miili ya wahajiri wanane waliokufa maji katika pwani ya mji wa Zarzis, kusini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hayo yameripotiwa na shirika la Hilali Nyekundu ambalo limeongeza kuwa, yumkini wahajiri hao waliokufa maji walikuwa kwenye boti iliyozama mwezi uliopita. Inaarifiwa kuwa, boti hiyo ilikuwa imebeba wahajiri 18. 

Jamaa za wahajiri hao wamekuwa wakifanya maandamano tangu wiki iliyopita katika mji wa Zarzis kusini mwa Tunisia, wakisisitiza kuwa serikali haijafuatilia kujua hatima ya wapendwa wao waliokuwa kwenye boti iliyozama.

Mongi Slim, afisa wa shirika la Hilali Nyekundu amesema, miili hiyo imepatikana na wavuvi waliofanya operesheni maalumu ya kusaka maiti za wahajiri hao.

Mwezi uliopita, Tunisia ilizima majaribio 22 ya wahamiaji haramu waliojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea pwani ya Italia, ndani ya saa 24. 

Mbali na kuwa kwake kwenye ncha ya bara la Afrika karibu na bara Ulaya, Tunisia inapakana pia na Libya na ni sehemu muhimu ya kuondokea wahamiaji wenye ndoto za kufika Ulaya na hasa nchini Italia. 

Ingawa mamlaka za Tunisia zimekuwa zikichukua hatua kali za kukabiliana na tatizo hilo, lakini majaribio ya uhamiaji haramu kutoka Tunisia hadi Italia hayaonyeshi dalili za kupungua.

342/