Main Title

source : Parstoday
Jumanne

18 Oktoba 2022

16:25:21
1314990

Maafa ya kizazi yaikabili Sudan baada ya mamilioni ya watoto kushindwa kwenda shule

Asasi za utoaji misaada ya kibinadamu zimetangaza kuwa, Sudan inakabailiwa na maafa ya kizazi kutokana na mamilioni ya watoto wanaopaswa kwenda shule kushindwa kufanya hivyo kutokana nna sababu mbalimbali.

Ripoti ya mashirika hayo ambayo yameupatia mfumo wa elimu nchini Sudan jina la "Maafa ya Kizazi" inaeleza kuwa, takribani watoto milioni 7 wameshindwa kwenda shule katika miaka ya hivi karibuni katikak maeneo ya vijijini.

Ripoti ya mwezi uliopita iliyotolewa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ilieleza kuwa, katika kila mabinti 10 wanne kati yao wameacha shule na katika kila watoto 10 wa kiume watatu kati yao wameacha masomo hali ambayo inatishia mustakabali wa kizazi ambacho kinatarajiwa kujenga taifa la kesho la Sudan.

Familia ambazo katika kipindi cha utawala wa Omar Hassan al-Bashir zilikuwa zikitaabika na kuteseka kwa matatizo makubwa ya kiuchumi hazikuwapeleka watoto wa shule.Kushadidi migogoro ya kisiasa, kiuchumi, kuibuka tena mapigano ya kikabila na kufungwa shule kwa muda mrefu wakati wa msambao wa virusi vya Corona ni mambo ambayo yalishadidisha matatizo yaliyokuwa yakiikabili sekta ya elimu nchini Sudan. Mbali na hayo, mamia ya walimu wamekuwa wakifanya mgomo mara kwa mara wakilalamikia mishahara midogo na mazingira mabaya ya kazi.

Aidha janga la mafuriko mwaka huu limesababisha hasara kwa zaidi ya shule 600 katikka maeneo mbalimbali ya Sudan na hivyo kuwa pigo jingine kwa sekta ya elimu ya nchi hiyo, na kupelekea kuakhirishwa mwaka wa masomo nchini humo.

Mwaka huu baada ya Afghanistan, nchi ya Sudan imeshika nafasi ya pili miongoni mwa mataifa 100 duniani ambayo sekta zao za elimu zimeathiriwa.


342/