Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

21 Oktoba 2022

16:47:49
1315898

Watu 150 wauawa kwa siku mbili katika mapigano ya kugombea ardhi Sudan

Kwa akali watu 150 wameuawa nchini Sudan katika mapigano ya siku mbili ya kikabila yaliyochochewa na mizozo ya ardhi katika jimbo la kusini mwa nchi hiyo la Blue Nile.

Ripoti zinasema kuwa, mapigano katika eneo lenye matatizo la Blue Nile nchini Sudan yalizuka wiki iliyopita baada ya kuripotiwa ugomvi kuhusu ardhi kati ya watu wa kabila la Hausa na makundi hasimu.

Mapigano hayo yamejikita zaidi katika eneo la Wadi al-Mahi yapata kilomita 500 kusini mwa mji mkuu Khartoum.

Siku ya Jumatano wakazi wa eneo hilo waliripoti milio ya risasi na kuchomwa moto baadhi ya nyumba.

Abbas Moussa, Mkuu wa Hospitali ya Wad al-Mahi ameaziambia duru za habari kwamba, "Jumla ya watu 150 wakiwemo wanawake, watoto, na wazee wamethibitishwa kuuawa kati ya Jumatano na jana Alkhamisi, huku watu 86 wakijeruhiwa katika ghasia hizo." 

Masoko na ofisi za serikali katika mji huo pia zimefungwa kwa sababu ya hali hii ya mambo na hivyo kutatiza upatikanaji wa bidhaa za mahitajio ya kila siku kwa wenyeji wa mji huo.

Mapigano kati ya makabila ya Hausa na Hamaj yalianza tangu Julai mwaka huu; ambapo tarehe 6 mwezi huu watu 149 waliuawa katika mapigano. Aidha watu wasiopungua 124 wamejeruhiwa hadi sasa huku wengine 64,800 wakilazimika kuhama makazi yao.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu(OCHA) imetangaza kuwa, ripoti ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kwamba, watu wanaokadiriwa 1,200 wamekimbia makazi yao kufuatia ghasia na mapigano hayo.

342/