Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

21 Oktoba 2022

16:49:52
1315901

Wanamgambo wa ADF washambulia vituo vya afya na kuua watu 7 DRC

Watu wasiopungua saba wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika eneo moja la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Norbert Muhindo, muuguzi katika kliniki moja mjini Maboya eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema wanamgambo hao walishambulia vituo viwili vya afya usiku wa kuamkia leo, na kuua watu saba, mbali na kumteka nyara muuguzi mmoja.

Muhindo amesema, "Wanaua hata wagonjwa. Waasi hao ni wanachama wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), lenye mfungamano na genge la ISIS katika eneo la Afrika ya Kati."

Kwa upande wake, Roger Wangeve, kiongozi wa asasi ya kiraia katka eneo la Bashu amesema mbali na wanagambo hao kufanya mauaji hayo ya kikatili, lakini pia wamechoma moto kituo cha afya cha Tinge na hospitali ya rufaa ya Maboya.

Ameongeza kuwa, wapiganaji hao baadaye walianza kuvishambulia vijiji katika maeneo hayo, huku wakiiba mali za wanaviiji na kuchoma moto nyumba zao.

Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia mgogoro kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi kwa muda wa miaka 20 iliyopita.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, makundi ya waasi yenye silaha yaliwaua zaidi ya raia 1,200 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri mwaka uliopita.


/342/