Main Title

source : Parstoday
Jumanne

25 Oktoba 2022

20:16:16
1317171

Askari 10, magaidi 18 wauawa katika makabiliano Burkina Faso

Wanajeshi wasiopungua 10 wa Burkina Faso wameuawa huku wengine zaidi ya 50 wakijeruhiwa, baada ya kundi moja la kigaidi kuvamia kambi ya jeshi katika eneo la Sahel nchini humo.

Jeshi la Burkina Faso limesema katika taarifa kuwa, wanamgambo hao wamevamia kituo cha Kikosi cha 14 cha jeshi la Burkina Faso katika mji wa Djibo mkoani Soum, kaskazini mwa nchi.

Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa, magaidi 18 wameangamizwa pia kwenye makabiliano hayo. Hata hivyo jeshi la Burkina Faso halijataja jina la genge hilo la kigaidi lililofanya shambulio hilo.

Limeeleza kuwa, kwa sasa limeongeza idadi ya wanajeshi katika eneo hilo, kwa ajili ya shughuli za uokoaji na operesheni za kujibu uvamizi huo wa magaidi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, askari wasiopungua 11 wa Burkina Faso waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulio jingine la kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo. Takriban raia 50 walitoweka kufuatia hujuma hiyo.

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani na imekuwa ikikabiliana na waasi wa makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida waliotokea nchi jirani ya Mali mwaka 2015. 

Mashambulizi ya waasi hao yamesababaisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha takriban watu milioni mbili kuyakimbia makazi yao.

342/