Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

27 Oktoba 2022

17:29:11
1317824

Mawaziri wa Uganda waanza kujifunza Kiswahili

Mawaziri wa Uganda wameazimia kuanza kujifundisha lugha ya Kiswahili, ambayo mbali na kuwa lugha ya kitaifa, lakini pia ni lugha rasmi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Uganda hivi karibuni iliidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya pili nchini humo baada ya Kiingereza, na kuifanya lugha hiyo kuwa ya lazima kufundishwa mashuleni.

Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rebecca Kadaga amesema kuwa, mawaziri wa Uganda sasa wataingia madarasani kwa saa chache kila asubuhi kujifunza Kiswahili, katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Kadaga ameeleza bayana kuwa, hatua hiyo inakusudia kuwawezesha mawaziri wote wa Uganda kufanya mikutano kwa lugha hiyo inayozungumzwa na watu zaidi ya milioni 200 katika pembe mbalimbali za dunia.

Waziri Kadaga alikuwa akizungumza katika Kongamano la Kila Mwaka la Mahakama ya Uadilifu ya Afrika Mashariki (EACJ) jijini Kampala.

Kadaga ambaye amewahi kuwa Spika wa Bunge la Uganda amebainisha kuwa, nchi hiyo ina furaha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo, na mkutano ujao wa majaji utakaofanyika mwezi ujao mjini Kampala.

Rais Yoweri Museveni kesho Ijuma anatazamiwa kulifunga kongamano hilo linalohudhuriwa na Majaji Wakuu, Mahakimu waandamizi na wanasheria wan chi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

342/